mwambelablog

Wednesday, 30 November 2022

RC CHALAMILA AWAONYA WAJUMBE WA BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA

 

Pichani:Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert John Chalamaila akimuapisha mjumbe wa baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Kyerwa.

Na Lydia Lugakila, 

Kagera.


Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert John Chalamaila amewaapisha wajumbe wa wanne wa baraza la ardhi na nyumba wilaya ya Kyerwa huku akiwaoya kukataa maelekezo ambayo yapo nje ya misingi ya kisheria yanayoweza kusababisha kukosekana kwa haki za watanzania.


Akizungumza baada ya kuwaapisha wajumbe hao ambao waliteuliwa hivi karibuni na waziri mwenye dhamana amesema wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria bila kuingiliwa na chombo chochote ili wawe wazalendo katika nchi yao.


"Fanyeni kazi zenu kwa weledi mkishakuwa na maelekezo kwa hiki kifanyike hivi mara kile vile ninyi rudini katika misingi ya sheria ili kujua kama kitu hicho kipo kisheria , fanyeni kwa mujibu wa taratibu epukeni kuelekezwa elekeza na kila mtu mtaharibu kazi yenu, na kuwakosesha haki watanzania" alisema.


Chalamila amesisitiza pia wajumbe hao kujiepusha na rushwa badala yake watoe haki na kupunguza mashauri ambayo yamerundikana katika mabaraza mengi bila sababu za msingi.


" Kumekuwa na mlolongo mkubwa wa kesi zinazohusiana na masuala ya ardhi na mirathi toeni elimu kuhusiana na mambo yatakayoweza kupunguza mashauri, tumieni Muhimili wa vyombo vya dini katika kupunguza masuala mengi yaliyo rundikana kwenye mabaraza" alisema 


Aidha Mwenyekiti wa baraza la ardhi wilaya ya Kyerwa Denis David amesema kuwa kuwepo kwa baraza hilo kumesaidia wananchi wengi kwani swali walikuwa wakifuata huduma hiyo wilaya jirani ya Karagwe.


Naye Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Rashid Muhamed Mwaimu amempongeza Rais Samia kwa kuwasogezea huduma hiyo ya kimahakama wilayani hapo kwani wananchi wake walilazimika kutembea umbali mrefu wa kilometa mia moja kwenda Karagwe ambapo pia alisisitiza watimize majukumu yao kizalendo 


Wajumbe walioapishwa ni Ester Mutafuta Ezra Lugakila Joyleth Godwin na Elias ambapo wameahidi kutenda haki huku kipaumbele cha kwanza likiwa ni kumpinga adui Rushwa .

OFISI YA WAZIRI MKUU KITENGO CHA MAAFA YATIMIZA AHADI KAGERA,

 



Na Lydia Lugakila,

 Kagera


Ofisi ya waziri mkuu kupitia kitengo cha maafa imeanza kutoa mafunzo ya uokoaji kwa wavuvi kutoka wilaya ya Bukoba Misenyi ikiwa ni hatua ya kuwaongezea uwezo wa kufanya uokoaji wakati yanapotokea majanga.


Akifungua mafunzo hayo mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la waziri mkuu alilolitoa baada ya kutokea ajali ya ndege precision Air  iliyotokea Novemba 6  mwaka huu ndani ya ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watun19 na 24 kunusurika.


Amesema kuwa  anaishukuru ofisi ya Waziri  Mkuu kitengo Cha maafa kuanza  kutoa Mafunzo hayo yatakayosaidia kuongeza ujuzi na uhodari katika uokozi kwa vikundi vya  wavuvi mkoani hapa huku akitoa wito kwa jamii ya Watanzania kuacha tabia ya kubeza juu ya juhudi zilizofanyika katika kipindi Cha ajali hiyo.


Naye mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Maafa kutoka Ofisi ya waziri mkuu, Luten Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa  wavuvi kutoka mkoani Kagera  walioshiriki kufanya uokoaji wanashiriki mafunzo hayo maalumu kwa kipindi cha  siku 7 ili waweze kuwapa mafunzo na uzoefu kutoka kwa wataalam ili kujua namna nzuri ya kuweza kumuokoa mtu anayepata ajali kwenye maji pamoja na utayari wa kukabiliana na majanga katika ziwa yanapotokea.



Ameongeza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kupunguza athari zinazojitokeza ziwani, ikiwa ni pamoja na kuokoa maisha ya watu na kupunguza upotevu wa mali wakati wa ajali.


Aidha kwa upande wao wavuvi hao akiwemo Hashim Rashid na Taufic Shariff wameishukuru serikali kwa mafunzo hayo kwani yatawanufaisha mbali na kuokoa wameongeza ufanisi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.


Wavuvi hao wamepata vifaa vya uokoaji vitakavyowasaidia kufanya kazi ya uokoaji kwa urahisi pamoja na kujifunza namna ya kuvitumia kuokoa watu ajali inapotokea ambapo

TET YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO NCHINI RWANDA

 


Kutoka Rwanda

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) pamoja na wajumbe wa kamati ya Kitaifa ya wataalamu inayosimamia uboreshaji wa Mitaala ya Elimumsingi, Sekondari ya Juu na Ualimu leo tarehe 29/11/2022 imetembelea Bodi ya Elimu ya Nchini Rwanda (Rwanda Basic Education Board) kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa  Mitaala yenye kujenga ujuzi.


TET ipo katika ziara nchini Rwanda kuanzia tarehe 28/11/2022 hadi 2/12/2022  kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho ya Mitaala yanayoendelea nchini.


Katika ziara hiyo Bi Joan Murungi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Elimu Rwanda (REB) aliwasilisha kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi hiyo na namna Rwanda inavyotekeleza mitaala inayojenga umahiri  ( Competence Curriculum Based)


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Kitaifa ya Mitaala Prof.Makenya Maboko amesema kuwa,Serikali ya Tanzania kupitia TET kwa sasa ipo inafanya maboresho ya mitaala itakayosaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira  kwa kumuandaa mhitimu mwenye ujuzi wa kujiajiri na kumudu maisha ya siku kwa siku.


"Tumekuja kujifunza nchini namna Rwanda inavyoandaa na kutekeleza Mitaala yenye kumjengea mwanafunzi ujuzi. Hili ndilo lengo la kufanya mapitio haya makubwa ya mitaala na kiu ya wadau wengi ni kuwa na mitaala itakayowawezesha wahitimu kuwa na ujuzi". Amesema Prof.Maboko.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amesema, uzoefu utakaopatikana utasaidia katika mapitio ya mitaala yanayoendelea.


"Kwa sasa tayari TET tumeandika rasimu ya mtaala na mihutasari lakini tumekuja hapa kupata uzoefu juu ya uandaaji na utekelezaji wa mitaala yenye kumjengea mhitimu uwezo wa kujiajiri na kumudu maisha ya kila siku" Amesema Dkt.Aneth.


Nchi ya Rwanda imefanya maboresho ya mtaala mwaka 2015 na kuweza kuwa na Mitaala inayozingatia ujenzi wa umahiri.

WAGANGA WAKUU WAELEKEZWA KUBORESHA USIMAMIZI WA UTENDAJI HUDUMA.

 

Pichani:NAIBU WAZIRI wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiongea na Waganga Wakuu wa Mikoa kuboresha usismamizi wa utoaji wa huduma za afya Nchini.

Na WAF - LINDI


NAIBU WAZIRI wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa kuboresha usismamizi wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma wanavyosimamia nchini.


Dkt. Mollel ametoa rai hiyo leo Novemba 30, 2022 wakati akifunga Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa Mikoa wanaosimamia Masuala ya Ukimwi nchini uliofanyika siku moja kabla kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.


"Tanzania imepiga hatua kubwa kuboresha huduma za afya, lakini juhudi za ziada zinahitajika kuboresha zaidi ubora wa huduma tunazotoa, hivyo natoa rai kwenu kwenda kusimamia hilo ” amesema Dkt. Mollel.


Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema kuwa, wakati huu ambapo Serikali inalenga kwenda kwenye Bima ya Afya kwa wote ni vyema kwa watendaji katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kuboresha zaidi huduma wanazotoa.


Kuhusu mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi, Dkt. Mollel amewapongeza watendaji pamoja na wadau wa Sekta ya Afya kusimamia vyema utekelezaji wa  afua za mapambano dhidi ya Ukimwi na kuiewezesha Tanzania kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kwa asilimia 62 toka mwaka 2010.


Aidha, Dkt. Mollel amewataka viongozi na watumishi kwa pamoja kuwajibika ipasavyo katika utoaji wa huduma bora ili kuweza kuokoa maisha ya Watanzania na kuwa na wananchi wenye afya njema wanaowajibika katika ujenzi wa nchi.


Sambamba na hilo ameendelea kusisitiza juu ya usimamizi mzuri wa dawa na kuhakikisha upungufu wa dawa haujitokezi katika vituo vyote vya kutolea huduma ili wananchi wasipate changamoto yoyote pindi wanapoenda kutafuta mahitaji. 


WAZIRI MKENDA APANIA MAGEUZI YA ELIMU

 

Pichani:Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa kikao cha pamoja cha Menejimenti ya Wizara na ile ya VETA jijini Dodoma.

Kutoka,DODOMA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na kuandaa mazingira ya kuhakikisha elimu ujuzi inapatikana.


Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja cha  Menejimenti ya Wizara na ile ya VETA chenye lengo la kujadili kwa pamoja rasimu ya  mkakati wa utekelezaji wa ujenzi wa VETA 63 za wilaya na moja ya mkoa.


Amesema moja ya eneo linaloangaliwa katika kutoa elimu ujuzi ni kupitia vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) hivyo ni   vizuri kuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha VETA 63 za Wilaya na moja ya mkoa ujenzi unaanza.


 "Nataka twende pamoja, katika kuweka historia hii; tunakwenda kufanya mageuzi makubwa ya elimu kwa kuhakikisha  tunatoa elimu ujuzi, sasa kazi ya mapitio ya Sera  na Mitaala inakwenda vizuri na tuko tayari kufanya wasilisho kwa ajili ya mjadala wa Kitaifa, sasa nataka huku kwenye ujenzi wa VETA 63 ambako elimu ujuzi inapatikana kuende kwa kasi na kwa  wakati ,"amesema Prof. Mkenda


Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizo hivyo  kutaka   mkakati wa kuhakikisha ujenzi unaanza mapema na kujengwa kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu zote husika.


Akizungumzia ujenzi wa Kampasi za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 kupitia Mradi wa HEET Mhe. Mkenda amewataka Wakandarasi waliopo wizarani kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji na kushirikiana na  na Vyuo Vikuu kujua mikakati iliyowekwa na Vyuo mama kuhusu ujenzi huo ili kazi iweze kwenda kwa haraka.


Akizungumzia maandalizi ya ujenzi wa VETA hizo Mhandisi George Sambali kutoka VETA  amesema mpaka sasa kati ya wilaya 63 zinazojengewa VETA wilaya 59 tayari zina maeneo.


CHANJO YA POLIO AWAMU YA NNE KUANZA KESHO TAREHE 1/12/2022.

 



Pichani: Afisa Program ya Chanjo Bi. Lotalis Gadau kutoka mpango wa Taifa wa Chanjo leo Novemba 30, 2022 wakati wa Semina elekezi kwa Wanahabari jijini Dodoma 


Na Deborah  Lemmubi - Dodoma.


Kampeni ya awamu ya nne ya Chanjo ya Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kuanza kesho ambapo watoto takribani 14,690,597 wanatarajiwa kupata chanjo hiyo.


Ambapo Kampeni hiyo inatarajiwa kuanza kesho December 1 hadi 4, 2022 na itafanyika nchi nzima , ikiwa Polio ni miongoni mwa magonjwa hatarishi zaidi kwa watoto ambapo virusi vya polio huvamia mfumo wa Neva na madhara yake husababisha kupooza au hata Kifo.


Hayo yamebainishwa na afisa Program ya Chanjo Bi. Lotalis Gadau kutoka mpango wa Taifa wa Chanjo leo Novemba 30, 2022 wakati wa Semina elekezi kwa Wanahabari jijini Dodoma inayohusu kutoa elimu kuelekea katika kampeni ya polio ambapo amesema kampeni hiyo itakuwa ni nyumba kwa nyumba.

Pichani:  Wanahabari leo Novemba 30, 2022 wakati wa Semina elekezi jijini Dodoma.


"Kwa utoaji wa chanjo za matone ya Polio ikilenga Watoto kuanzia Umri chini ya Miaka mitano sambamba na Timu za wachanjaji ambapo kutakuwepo na waangalizi wa kujitegemea katika Kila Mkoa nchini ili kukamilisha zoezi hilo"


Aidha Bi Lotalis ametaja njia za maambukizi ya ugonjwa huo sambamba na dalili ikiwa ni pamoja na homa, uchovu, maumivu, ya kichwa, kutapika, kukakamaa shingo na maumivu ya Viungo.


“Ugonjwa huu huambukizwa kwa kuingia mwilini kwa njia ya mdomo, kunywa Maji,au chakula ambacho kimechafuliwa na kinyesi kutoka kwa Mtu aliyeambukizwa virusi hivyo na virusi huongezeka ndani ya utumbo na hutolewa na mtu aliyeambukizwa kwenye kinyesi, ambacho kinaweza kupitisha virusi kwa wengine”


Pia ameeleza Hali ilivyo kwa sasa juu ya ugonjwa wa Polio katika maeneo mbalimbali ndani ya Bara la Afrika.


“ambapo amesema, Zambia tayari kuna kisa kimoja, wenyewe wanajiandaa na awamu ya Tatu,Msumbiji wa visa 8 na wanajiandaa na awamu ya 6 Malawi wana kisa 1 na wanajiadaa na awamu ya 5,na kwetu Tanzania tunamshukuru mungu bado hatujapata kisa, lakini bado hatujalemaa, bado tunaendelea na ufuatiliaji kwa kuchukua Sampuli kuhakikisha kwamba tunapeleka maabara mwisho wa siku watoto wetu wawe salama.DRC CONGO bado kuna vimlipuko vya hapa na pale lakini ambao tulienda nao sambamba tokea tunaanza mwanzo ni Malawi, Msumbiji, Zimababwe na Zambia”


Pia ameeleza mikakati inayotumika katika kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa huo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni za kutoa elimu itakayoambatana na utoaji wa Chanjo.


“Tunachojitahidi ni kuonyesha kwamba tunaimarisha utoaji wa chanjo za kila siku kuhakikisha kwamba watoto wetu wanakamilisha Ratiba zao za chanjo ili endapo hata Kirusi kikija kikimkuta mtoto ameshapata kinga kamili kinakuwa hakina nafasi na kwa awamu hii tunalenga kuwafikia watoto wapatao Millioni 14 laki sita na Tisini, Mia tano Tisini na Saba kwa awamu hii ya nne”


Bi lotalis amehitimisha kwa kusema kuwa zoezi hili litafanyika kwa kupita nyumba kwa nyumba na kisha nyumba ambayo itakuwa imepata chanjo itawekwa alama ya Tiki ili kuonesha tayari imekwisha kupata huduma ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo na kuepusha usumbufu wa foleni na upotevu wa muda.

Monday, 28 November 2022

WACHIMBAJI WADOGO WASHAURIWA KUPATA TAARIFA ZA KIJIOLOJIA KTOKA MAENEO SAHIHI

 

Na Deborah  Lemmubi - Dodoma.


Wachimbaji wadogo wa Madini Nchini wameshauri kuwa na tabia ya kupata taarifa za Kijiolojia maeneo ambayo sahihi hasa Taasisi ya Jiolojia Tanzania ili kuepuka Uchimbaji wa kubashiri na uharibifu wa Mazingira.


Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi Uendelezaji wa wachimbaji wadogo kutoka Wizara ya Madini Mhe Francis Mihayo akiwa katika Jukwaa la sekta ya Uziduaji lililoandaliwa na Shirika la HakiRasilimali lililofanyika Jijini Dodoma.



"Kwa ushauri Watanzania wapende kutafuta taarifa maeneo ambayo ni sahihi,kwa fursa hii napenda nitambulishe kuwa tuna Taasisi ya Jiolojia (GST) inawezekana hawaijui au hawajui majukumu yake, lakini kikubwa wao ndio wana jukumu la kufuatilia taarifa za kijiolojia"


"Na kuongeza kuwa, Tukisema taarifa za kijiolojia ni taarifa za Madini yote ambayo yanapatikana Tanzania kwani Taasisi hii wanatengeneza ramani za madini yote,wana taarifa zote na wanafanya Tafiti zote, Mfano ukitaka kujua Dhahabu inapatikana wapi wao watakwambia Dhahabu inapatikana mahali fulani iwe ni Kanda ya Ziwa au kwingineko"


Aidha Mhe Mihayo amewataka wachimbaji wadogo kuendelea kutunza Mazingira katika maeneo ya kazi zao.


"Suala la kutunza Mazingira ni muhimu kwa Wachimbaji hawa hasa pale anapotaka kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine ni vema akahakikisha pale anapotoka Mazingira yapo sawa kwa kufukia mashimo yote ikiwezekana apande hata miti"


Kwa upande wa CPA Ludovick Uttoh ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji ya Uwazi na Uwajibikaji katika sekta ya Uziduaji (MSG) amesema Uwazi na Uwajibikaji wa kweli ni muhimu katika kukuza ongezeko la Uchumi wa Nchi kupitia sekta hii ya Uziduaji.


"Katika miaka mitatu/minne iliyopita uchangiaji wa hii sekta kwa uchumi wa Nchi ni asilimia 3.2, mwaka jana ilifika asilimia 7 na kwa lengo itakapofika 2025 matarajio na mipango ya Serikali kwamba hii sekta iweze kuchangia kwa asilimia 10, lakini hatutafika huko kama hakutakuwa na Uwazi na  Uwajibikaji wa kweli katika usimamizi wa hii sekta"


Naye Eng Theonista Mwasha ambaye ni Mwanamke wa kwanza katika Sekta hii ya Uziduaji na Katibu Mtendaji kutoka Taasisi ya kuendeleza Uchimbaji mdogo Tanzania amesema Wanawake wanachangamoto ya kutojiamni katika sekta hii ya uziduaji inayopelekea Wanawake kutofaidika kama inavyotakiwa.


"Wanawake wamekuwemo katika hiyo sekta kwa muda mrefu lakini wameshindwa kufaidika kama inavyotakiwa,kwasababu ya uelewa pia wamejiona wao wako nyuma kama sekta nyingine. Kimila na Desturi Mwanamke anajiona kwamba hiki mimi siwezi kwahiyo tunawajengea uwezo wa kujiamini ili kama wameamua kufanya kazi wafanye kwa nguvu zao zote na akili zao zote pia wajiamni"


Jukwaa hili la Uziduaji ambalo kuratibiwa na Shirika la HakiRasilimali hufanyika kila mwaka na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hii ili kujadili mambo tofauti ikiwemo kuangazia changamoto wanazopata wachimbaji wadogo na kuona  namna ya kuzitatua.

Friday, 25 November 2022

WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUTUNZA SIRI ZA SERIKALI KWA MASILAHI YA NCHI

 

MWENYEKITI wa Tume ya Watumishi wa Umma ,Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya chamwino Mkoani Dodoma wakati wa ziara ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma walipotembelea Halmashauri hiyo.

Kutoka Dodoma

MWENYEKITI wa Tume ya Watumishi wa Umma ,Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, amewataka watumishi wa Umma kutunza Siri za Serikali  ili kulinda Maslahi ya Nchi.

Hayo ameyasema wakati wa ziara ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma walipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

Jaji Mstaafu Mhe. Kalombola,amewahimiza watumishi kuwa waminifu katika kulitumikia Taifa kwa kulinda maslahi kwa kutunza viapo vyao na kuacha kuvunjisha siri za utumishi.

”Kuna baadhi ya watumishi wa Serikali wamekuwa na mmomonyoko wa maadili kwa kuvunjisha siri za Serikali hivyo tunawaomba waache tabia hiyo walinde viapo vyao kwa kusimamia maadili ya utumishi wao.”amesema Jaji Mstaafu Mhe. Kalombola 

Aidha Jaji Mstaafu Mhe. Kalombola amewataka watumishi kuwa wabunifu katika kazi zao ili kuongeza mapato na kujiletea maendeleo kwenye Taasisi zao  na wachukulie changamoto kama sehemu ya kazi zao.

Vilevile Jaji Mstaafu Mhe. Kalombola ameeleza kuwa Tume  hiyo katika majukumu yake imejiwekea utaratibu wa kutembelea Taasisi pamoja na maeneo mbalimbali ya Serikali kwa lengo la kuelimisha,kuelekeza uwajibikaji na kubadilishana uzoefu ili kuboresha uendeshaji wa usimamizi na maswala ya utumishi kwa mujibu wa sheria.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani inawathamini sana watumishi wa Umma Kwa Mchango mnaoutoa katika kuwahudumia wananchi kwenye kuleta maendeleo yao”amefafanua Jaji Mstaafu Mhe. Hamisa

Kwa Upande wake Kamishna wa Tume, Mhe. Nassor Mnambila amewashukuru viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Chamwino kwa muitikio wao na mapokezi yao makubwa kwenye ziara hiyo yenye lengo la kutoa mrejesho na kujifunza namna ya ukusanyaji wa mapato.

“Tunawashukuru viongozi wa Halmashauri hii kwa mapokezi yenu na kukubali kuja kwenu kujifunza namna mashine hizi za posi zinavyotumika kukusanya mapato lakini pia tuwapongeze kwa ujenzi wa madarasa Matatu mukishirikiana na wananchi”. Amesema Mhe.Nambila

Katika Ziara ya Makamishna wa Tume katika Halmashauri ya Chamwino ilikuwa na  lengo la kujifunza, kuelimisha na kuwakumbusha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

WAGANGA WATOE DAWA KULINGANA NA MAJIBU YA MAABARA

Pichani: Mganga Mkuu wa Serikali (CMO),Prof. Bi. Tumaini Nagu akizungumza katika kongamano la wiki ya Kampeni ya Kuzuia Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa, Jijini Dar es Salaam ambapo lilianza 18-25 Novemba mwaka huu


Na Andrew Chale,

Dar es Salaam.

WIZARA ya Afya kupitia kwa Mganga Mkuu wa Serikali [CMO], Prof. Bi. Tumaini Nagu ametoa maagizo kwa Waganga na Madaktari nchini kutoa dawa kwa wagonjwa kulingana na majibu ya Kimaabara ilikutambua dawa gani sahihi ya kutibu ugonjwa husika kuepuka usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.


Ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati wa wiki ya kampeni ya kuzuia usugu wa vimelea dhidi ya dawa za Antibiotiki inayoadhimishwa kila mwaka 18-24 Novemba ambapo mwaka huu kauli mbiu ‘’Kwa pamoja tuzuie usugu wa vimelea dhidi ya dawa’’, ambapo Prof. Nagu amesema usugu wa dawa husababishwa na mambo mengi ikiwemo kutofuata usahihi wa matumizi na pia kukwepa kutumia wataalam wa hospitali.


‘’kwa sasa usugu wa vimelea vya dawa umeongezeka moja wapo ni kutotumia dawa kwa usahihi, mfano mtu unaambiwa utumie dawa kwa siku tano, wewe unatumia kwa siku mbili unapopata nafuu unaaacha hapa unajenga usugu kwa sababu havijaisha mwilini mwako.


Lakini pia pia kutumia madawa kabla ya hujapimwa,

Wapo wanaoenda duka la dawa hawajaonwa hata na Daktari,  wao wanaenda kuchukua dawa bila kupimwa pindi wanapojisikia vibaya wanapewa hizi dawa za Antibiotiki.


...Na hapa naomba niwaase wananchi wote, unapojisikia vibaya tumia huduma zetu za afya.


Uende hospitali yoyote iliyopo jirani, umuone daktari akupime, na ukiwa umeonekana na vimelea vya ‘infection’ atachukua 'sample' atapeleka maabara vitapimwa, kwa hiyo katika hili niwaombe pia Waganga madaktari, watumie hizi huduma za maabara kuangalia kama mtu anaugonjwa ilikujua anatumia dawa gani katika kukabiliana na ugonjwa husika.’’ Alisema Prof. Nagu.


Aidha, ameongeza kuwa, Waganga watoe madawa sahihi kulingana na ugonjwa husika, na pia ameomba kuwa watoe dawa hizo kulingana na majibu ya Maabara akisistiza.


Aidha, Prof. Nagu amesema kwa sasa usugu kwa Tanzania unakadiriwa kuwa kati ya Asilimia 59.8 hadi 60  hii ni wastani ambapo amebainisha kuwa, vimelea vipo aina nyingi na dawa zipo za aina tofauti, hivyo ametoa raia dawa za Antibiotiki ziachwe kutumika kiholela na zaidi zitumike kulingana na ushauri wa kitaalam.


‘’Vimelea vikiwemo mwilini lazima tutumie Antibiotiki, lakini tutumie kwa uangalifu kulingana na wataalam, lakini pia tuweke mazingira ya usafi ya kujilinda ikiwemo kuosha mikono mara kwa mara, kusafisha Vyoo na usafi wa mwili  ilikuepuka magonjwa,


Hivyo niwaombe watu wote wananchi, tujaribu kujikinga kwa kuboresha usafi wa mazingira, kuosha vyoo na vitu vingine vingi katika hali ya usafi.’’ Alisema Prof. Nagu.


Aidha, amesema usugu wa dawa unatofautiana  kulinagana na utumiaji wa madawa,katika  hospitali moja na nyingine kulingana na mpangilio kazi wao wa utoaji wa madawa kwa wagonjwa wao kulingana na matumizi ya hospitali husika.


Katika kongamano hilo ambalo linatarajiwa kufikia tamati leo, wadau mbalimbali wameweza kuwasilisha mada za kibobezi katika sekta ya afya ikiwemo ya madawa ya binadamu na mifugo dhidi ya kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.


Mwisho.

WILAYA YA KYERWA YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO

 


Na Lydia Lugakila

Kutoka Kyerwa.


Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imempongeza Rais Samia kwa kuwaletea miradi mbali mbali ya maendeleo ambapo wanatarajia ifikapo Novemba 25 ya mwaka mahakama mpya wilaya itaanza kufanya kazi baada ya kukamilika jambo litakalowaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika wilaya jirani ya Karagwe.


Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili taarifa mbali mbali za robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023 kilichofanyika ukumbi wa Rweru mkuu wa wilaya ya Kyerwa Rashid Mohamed Mwaimu amesema kuwa juhudi za Rais Samia zimeifanya wilaya hiyo kuendelea kung'ara kwani kwa kipindi cha muda mrefu wananchi wake wamekuwa wakifuata huduma ya mahakama katika wilaya jirani ya Karagwe ambapo walilazimika kutumia mwendo wa kilometa 80.


"Novemba 25 mwaka huu mahakama yetu inaanza kufanya kazi namshukuru Rais Samia kwa kutusogezea huduma hii, nawashukuru wanakaragwe kwa kutufadhili kwa kipindi chote hicho sasa wilaya yangu inajitegemea inasimama kwa miguu yote" alisema Mwaimu.


Aidha Mwaimu ameongeza kuwa ifikapo Desemba mosi mwaka huu wanatarajia kuanza baraza la nyumba la wilaya baada ya kukamilika kwa ujenzi itasaidia  wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda wilayani Karagwe kufuata huduma hiyo.


Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya amewaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwani hadi sasa wilaya ya Kyerwa imeongezewa nguvu kazi katika sekta mbali mbali ikiwemo afya, Elimu huku akimuomba Rais Samia kuiangalia wilaya hiyo kwa macho mawili kutokana na kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa watumishi.

TUKO TAYARI KWA MJADALA WA KITAIFA KUHUSU MAPENDEKEZO YA SERA YA ELIMU_ WAZIRI MKENDA

 

Pichani: Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolf  Mkenda akiteta Jambo na Makamo wa Rais Mhe. Philipo Mpango katika Mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria Jijini Mwanza.


Kutoka Mwanza 


Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu Msingi yamekamilika na yanasubiri mchakato wa ndani ya Serikali ili kupata ridhaa ya rasimu zilizoandaliwa  kupelekwa kwa wadau kwa mjadala wa kitaifa.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolf  Mkenda wakati akizungumza katika Mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria Jijini Mwanza, ambapo amesema kuna mambo makubwa ambayo yamependekezwa na wadau mbalimbali.


Prof. Mkenda  amefafanua kuwa  utekelezaji wa kazi hiyo umeendelea kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Maaskofu, Mashekhe, walimu, wenye shule binafsi pamoja na wataalamu kutoka nje ya nchi ili kupata uzoefu kutoka katika nchi zilizoleta mageuzi ya elimu na kufanikiwa na zile ambazo hazikufanikiwa. 


"Tumekamilisha rasimu ya mapitio ya Sera, ina mapendekezo mengi makubwa, tunachosubiri sasa ni mchakato wa ndani wa kupitia mapendekezo hayo kabla hatuyatangaza rasmi kwa ajili ya mdahalo wa kitaifa na hatimae mchakato wa maamuzi uweze kufikiwa ndani ya Serikali," amesema Prof. Mkenda.


Akitolea mfano jambo moja ambalo limeguswa katika mapitio ya Sera ni suala la walimu  kupewa kipaumbele katika ubora na suala la mafunzo endelevu kazini ambalo hata sasa suala hilo la mafunzo kazini limeshaanza na linaendelea.    


"Katika mapitio ya Sera walimu waliopo wataendelea kupewa mafunzo kazini, ambayo tayari wameshaanza kuyapata na walimu wapya tutaona vigezo katika mapitio ya Sera kuhakikisha tunakuwa na walimu bora wa kuendeleza elimu yetu," amefafanua Prof. Mkenda.


Aliongeza kuwa kazi ya kupitia mitaala nayo inakwenda vizuri  pamoja na kuwa kwa kawaida hapa nchini kazi hiyo ilikuwa hailepelekwi katika ngazi ya maamuzi kutokana na kuwa ni kazi ya kitaalamu zaidi, lakini kwa mageuzi haya ya elimu italetwa kwenye ngazi za juu na kisha kujadiliwa na umma wa Watanzania.


Ameongeza kuwa mageuzi hayo ya mitaala yatafanyika pia katika ngazi ya  Elimu ya Juu ambapo huko utaangaliwa zaidi ubora wa elimu.

DKT.HASSAN ABASI MGENI RASMI PRICESS DAY

 

Pichani:Ni Mtendaji Mkuu wa shule ya Vipaji ya Fountain Gate academy Bwana Thabiti Kandoro wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.


Na Deborah  Lemmubi - Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbas anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika Siku maalum ya Timu ya Wanawake ya Fountain Gate Accademy itakayofanyika tarehe 27/11/2022 inajuyojulikana kama a Princess Day.


Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa shule ya Vipaji ya Fountain Gate Bwana Thabiti Kandoro wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu siku hiyo maalum ya Timu ya Wanawake.


Aidha Bwana Kandoro amesema katika kusherehekea siku hiyo wameialika Timu kutoka Nchini Uganda ya Lady Dovu na imethibitisha kushiriki, pia kutakuwa na uzinduzi wa Jezi,kutambulisha malengo ya Msimu,Maendeleo na kutambulisha Wachezaji wa Timu ya Wanawake Fountain Gate kwa msimu wa 2022/2023.


Pia Kandoro amesema Fountain Gate kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi kuu ya wanawake [WPL] haya ni mafanikio makubwa wanayojivunia kutoka kwa vijana hawa wa  shule yao.


Sambamba na hilo Kandoro amesema  Pamoja na mambo mengine  kituo hicho wamepokea watoto zaidi ya mia moja kutoka Mikoa mbalimbali Kwa ajili ya kuwapatia Elimu na kuwaendeleza vipaji vyao walivyonayo vya  mpira.


Katika kuendelea na maandalizi ya kuadhimisha ya siku hiyo Timu ya Fourntain Gate na Uongozi mzima watatembelea watu wenye mahitaji maalum kama vile Vituo vya Wazee,Vituo vya kulelea Watoto,Hospital na Nyumba za kuwatunza watu walioathirika na Dawa za kulevya.

Monday, 21 November 2022

RUSHWA YAGEUKA CHANGAMOTO UCHAGUZI CCM MKOA

 

Pichani:Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Dkt Daniel Chongolo akizungumza na wanahabari pichani hawapo.

Na Deborah Lemmubi - Dodoma.


Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu wafutiwa Uchaguzi kwasababu ya uwepo wa tuhuma za Rushwa.


Hayo yamesemwa mapema leo hii Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Dkt Daniel Chongolo alipokuwa akizungumza na wanahabari kutoa Taarifa juu ya chaguzi zinazoendelea ndani ya chama cha CCM kwa ngazi ya Mikoa.


"Tumefuta uchaguzi wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu kwa sababu ya kuwepo kwa tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wagombea,nimeshatuma timu huko leo siku ya tatu kufanya uchunguzi wa kina wakimaliza wakatuletea ripoti tutafanya uamuzi"


Aidha Dkt Chongolo amesema kuwa wamesimamisha Uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa kwa Mkoa wa Mbeya na Arusha nayo changamoto ikiwa ni tuhuma za Rushwa.


"Pili tumesimamisha Uchaguzi nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mkoa wa Mbeya kwa sababu ya tuhuma mbalimbali ikiwemo za rushwa na lenyewe tunalifanyia uchunguzi wa kina na tukilikamilisha tutatoa taarifa ya uamuzi wa Chama"


"Tatu tumesimamisha uchaguzi kwa nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mkoa wa Arusha naye tatizo ni hilo hilo changamoto zikiwemo za rushwa,tukikamilisha uchunguzi tutatoa taarifa ya uamuzi wa Chama na kuendelea au kuruhusu Uchaguzi uendelee"


Pia Chongolo amezungumzia malalamiko yaliyojitokeza kwa wagombea kwenye uchaguzi uliofanyika jana Mkoa wa Magharibi kisiwani Zanzibar ambapo amesema.


"Lakini pia kuna uchaguzi uliofanyika jana Mkoa wa kichama Magharibi Zanzibar  ambapo kulikuwa na malalamiko ya baadhi ya wagombea na wajumbe wakieleza kuhusiana na tukio la moja ya wanachama kuchukua boksi la kura na kwenda nalo kwenye chumba kilichoandaliwa kwaajili ya kuhesabia kura, sasa kwa sababu tuna haya malalamiko tunataka kujua walilenga kuhesabu kura au walikuwa na lengo lingine na tutafuatilia tukithibitisha tutachukua uamuzi"


Mwisho amewaasa wagombea wanaotumia hila katika Chaguzi zinazoendelea wakionesha kuwa wao ni wagombea maalum na wanaojulikana na viongozi wa ngazi za juu.


"Changamoto tunayopitia hivi sasa ni baadhi ya wagombea au wapambe wao kujionesha kuwa wao ni maalum kuliko wengine na wao ndio wanaojulikana na viongozi wa juu kuliko kuliko wengine wapo wanaojiita wagombea wa Katibu mkuu,wapo wanaojiita wagombea wa Makamu Mwenyekiti, wapo wanaojiita wagombea wa Mwenyekiti na wapo wanaojiita wagombea wa Wajumbe wa Kamati Kuu,waache kutumia hila hiyo katika Uchaguzi"


Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha unaendelea kama kawaida pamoja na nafasi zingine za wajumbe,wawakilishi wa Chama kwenda kwenye jumuiya nyinginezo bado unaendelea kama kawaida.

TUWAPATIE VIJANA NA WATOTO WA KIUME MALEZI BORA NA ELIMU YA STADI ZA MAISHA

 

Pichani: Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule

Na Deborah Lemmubi - Dodoma.


Wito umetolewa kwa jamii kutosahahu watoto na vijana wa kiume katika kuwapatia malezi bora na elimu ya stadi za maisha ili kujenga familia imara na bora katika Nchi yetu.


Wito umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule akiwa mgeni rasmi akimwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson katika Kongamano la wanawake na mabinti lililolenga kuwapa uelewa wa kuangazia fursa za kiuchumi kwa wanawake wa Jiji la Dodoma lililoitwa Mega Ladies Talk Show, na kubeba kauli mbiu inayosema Born ti Win and Shine,lililoandaliwa na umoja wa VCC Super Ladies kutoka kanisa la VCC(Victory Celebration Centre) lililopo Jijini Dodoma.


"Aidha napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa jamii kutowasahau watoto na vijana wakiume katika kuwapatia malezi bora na elimu ya stadi za maisha ili kujenga familia imara na bora katika Nchi yetu"


"Na kuongeza kuwa. Tukishirikiana kwa pamoja tutakuwa na vijana wa kiume hodari,wachapakazi na wenye hofu ya Mungu. Hii itapunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukiukaji wa maadili,uhalifu na uvunjifu wa amani. Sote ni mashahidi wa kuibuka kwa makundi ya vijana wahalifu maarufu kama kama panya-road ambao ukiwatazama bado ni wadogo kiumri na hawa ndio tunaowategemea kuanzisha familia na kujenga Taifa imara"


Aidha RC Senyemule amesema Nchi haiwezi kuwa na maendeleo iwapo amani na ushirikianao katika ngazi ya familia havipo. Na familia haiwezi kuwa na amani iwapo mahusiano katika ndoa ni mabaya au ikiwa hali za kiafya na uchumi sio nzuri.


"Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi mahiri wa Mama yetu Mpendwa Mhe Samia Suluhu Hassan Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikisisitiza amani na ushirikiano bana yetu ambayo ni nguzo ya Maendeleo kwa Taifa. Lakini tujue pia kuwa Nchi haiwezi kuwa na Maendeleo iwapo amani na ushirikiano katika ngazi ya familia havipo. Familia haiwezi kuwa na amani iwapo mahusiani katika ndoa ni mabaya au ikiwa hali za kiafya na uchumi sio nzuri"


Pia RC amekumbusha kuwa hata katika maandiko matakatifu mwanamke ameonekana kuwa kiungo cha familia na jamii kwa namna mbalimbali. Kwa mfano katika kitabu cha Samweli wa kwanza sura ya 25 kinamtaja Abigaili aliyetumia Busara na Hekima ili mumewe asiangamizwe pia Mwanzo 1:26 inaonesha kuwa Wanawake na Wanaume ni viumbe wa thamani hivyo hawapaswi kujidharau.


"Mwanamke aliyeelimika anayo nafasi kubwa katika ngazi ya familia,jamii na hata Taifa ya kuchochea Maendeleo. Kwa kuzingatia hilo Mhe Raisi amekuwa akiteua wanawake wenye uwezo katika ngazi za juu za maamuzi kwa kuwa anajua umuhimu wao"


"Hata katika maandiko matakatifu mwanamke ameonekana kuwa kiungo cha familia na jamii kwa namna mbalimbali. Kwa mfano katika kitabu cha Samweli wa kwanza sura ya 25 kinamtaja Abigail mwanamke aliyekuwa ameolewa na mwanaume katili lakini akatumia busara na hekima kuomba radhi kwa Mfalme kwa niaba ya mume wake hatimaye familia yake haikuangamizwa. Pia katika kitabu cha Mwanzo 1:26 inaonesha kuwa wanawake na wanaume wote ni viumbe wa thamani na wenye uwezo,hivyo mtu awaye yeyote hatakiwi kujidharau"


Sambamba na yote ametoa pongezi kwa viongozi wa dini kwa kuwa na ushirikiano na Serikali katika Maendeleo ya Elimu na Afya.


Vile vile nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa madhehebu ya dini kwa kushirikana na Serikali katika nyanja mbalimbali za Maendeleo ikiwemo elimu na afya"


Kwa uapnde wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste na mlezi wa maono ya kongamano hili Mchungaji Dkt Baraka Kihoza amesema kama kauli mbiu ya Kongamano hili inavyosema Born to Win and Shine yani Kushinda na Kung'ara hivyo kung'ara ni pamoja na mwanamke kung'ara kiuchumi.


Kongamano hili la Mega Ladies Talk Show ni maono ya Mchungaji msaidizi wa Kanisa la VCC Josephine Kihoza,yakiwa ni maono yenye kutamani mwanamke amalize mwaka akiwa na matumaini mapya na ushindi hasa katika nyanja ya kiuchumi kama Mungu anavyotaka watu wote wawe wenye furaha.

Sunday, 20 November 2022

TAASISI NA VITUO VYA AFYA WAAGIZWA KUTEKELEZA MPANGO WA TAIFA WA KUPAMBANA NA USUGU WA DAWA DHIDI YA VIMELEA MBALIMBALI

 

Pichani: Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalaghe Jijini Dodoma Katika wiki ya Kampeni ya kuzuia Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa za Antibiotiki 


Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa agizo kwa taasisi na vituo vyote vya kutolea huduma za afya kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kupambana na Usugu wa Dawa dhidi ya vimelea mbalimbali  antimicrobial(2023-2028) huku akiwataka Matabibu kote nchini kuandika dawa kwa kufuata mwongozo wa matibabu wa mwaka 2021 na kutumia majina halisi ya dawa (generics) na kwa usahihi.


Agizo hilo limetolewa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalaghe Jijini Dodoma Katika wiki ya Kampeni ya kuzuia Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa za Antibiotiki ambapo ametoa ametaka Watoa dawa (Dispenser)  kusoma na kuelewa maelekezo ya matabibu na kutoa maelekezo sahihi kwa wagonjwa. 



Aidha kutokana na Ripoti iliyotolewa na 

Benki ya Dunia mwaka 2017, imeonesha kuwa ifikapo mwaka 2050 uchumi wa Dunia utapungua kwa asilimia (3.8%) na kwamba kiasi cha dola za Marekani trilioni 3.4 zitapotea ifikapo mwaka 2030 kutokana na tatizo hilo. 


''Aidha, ripoti hiyo imeeleza kuwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania zinaathirika zaidi ambapo 

kiasi cha dola za Marekani bilioni tisa (9) zitatumika kila mwaka kupambana na 

usugu wa vimelea dhidi ya dawa hizo''.Dkt Shekalaghe


Katika Hatua nyingine Dkt Shekalaghe amewaasa wananchi katika wiki hii ya maadhimisho kujifunza juu ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa na ni kitu gani kinawapasa kufanya kuimarisha afya zao. 


Njia nzuri na rahisi kuzuia na kutokomeza usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni kwa jamii na wataalam wa Sekta ya afya ya binadamu, Wanyama na Mazingira kutimiza wajibu wetu katika kuhakikisha kuwa dawa sahihi inatolewa na kutumika tu pale inapohitajika. 



FUATENI UTARATIBU UJENZI WA MIRADI YA ELIMU’

 

Pichani: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki wakati wa kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora mkoani Tabora.


Kutoka TABORA


WAKURUGENZI wa Halmashauri nchini wametakiwa kutekeleza miradi ya sekta ya elimu kwa kufuata miongozo ili kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza pindi miradi hiyo ikitekelezwa kinyume na utaratibu.


Hayo yameagizwa leo Novemba 19, 2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki wakati wa kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora mkoani Tabora.


Amesema ni vyema wakurugenzi wakahakikisha wanafuata maelekezo yanayotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI juu ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na kuwa tofauti na hapo wanatakiwa kuomba muongozo wa mabadiliko kabla ya kuendelea na mabadiliko.

.

“Endapo mna maoni tofauti na maelekezo na miongozo iliyotolewa kabla hujabadilisha au kufanya utekelezaji tofauti ofisi iko wazi tuzungumze.”amesisitiza Waziri Kairuki


Amesema  kuna Halmashauri ambazo zimeanza kutekeleza wanavyoona wao, sidhani kama itajitokeza hapa Tabora, una maoni tofauti wasilisha maoni kabla hujafanya tofauti, kila mtu akijiamulia anaenda anavyotaka hatutakuwa na utaratibu.


Aidha, Waziri Kairuki amesisitiza ushirikishwaji wa jamii na viongozi katika kuibua miradi inayopaswa kutekelezwa katika Halmashauri husika ili fedha zipelekwe eneo lenye uhitaji.


“ Tujitahidi kuwashirikisha maafisa elimu, madiwani wetu, wabunge pamoja na wananchi wengine ili kupata orodha sahihi, ili tukifanya maandalizi yetu ya kuleta fedha za ujenzi wa shule za msingi au kama ni ukarabati basi tunauhakika tunazileta kwenye maeneo yenye uhitaji, tusipofanya hivyo itakuwa ni mtihani.” amesema


Mabalozi wa Tanzania Wakabidhiwa Vitabu vya Kufundishia Kiswahili Nje ya Nchi

 



Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake Said Yakubu imekabidhi vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa Mabalozi wa Tanzania kwa ajili ya kufundishia lugha ya kiswahili nje ya nchi kwenye hafla ya mkutano wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania ulioanza Novemba 14, 2022.


Akizungumza wakati akitoa mada kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Ubidhaishaji wa Lugha ya Kiswahili kwa mabalozi wa Tanzania na Watumishi waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Naibu Katibu Mkuu Said Yakubu amesema mabalozi wana nafasi kubwa ya kukuza na kukiendeleza kiswahili katika nchi wanazoziwakilisha na kupitia mpango huo utawasaidia kujua njia zitakazosaidia kukuza lugha ya kiswahili.


“Lugha ya kiswahili ni lugha ya Dunia kutokana na kuongezeka kwa kasi ya watumiaji wengi duniani na hiyo imethibitishwa na UNESCO baada ya kuitangaza Julai 7 kuwa maalum kwa ajili ya kusherehekea kiswahili duniani,” alisema Yakubu.


Amesema kiswahili kwa sasa kina wazungumzaji takribani milioni 500 na vituo takribani 150 vinavyofundisha lugha hiyo ambapo watanzania 2000 wamepata ajira za kuweza kufundisha katika vituo hivyo. Huku akisema hiyo ni dalili kwamba kiswahili kinakubalika duniani na kinakuwa kwa kasi.


Ameongeza kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa bungeni alisema ili kukuza kiswahili balozi zote zijenge vituo vya kufundishia kiswahili ili iwe nguzo ya kujenga diplomasia ya uchumi na Watanzania na kuongeza wigo wa watumiaji wa kiswahili duniani.


Naye Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi amesema mkakati huo ni wa miaka 10 na unatarajiwa kutekelezwa kati ya mwaka 2022-2032.


Katika Hafla Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imekabidhi Tuzo kwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Samwel Shelukindo kwa kutambua mchango wake katika kukuza na kueneza kiswahili duniani.


Hafla hiyo iliwashirikisha Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Wizara ya Elimu.

NTDS YAWANOA WATENDAJI NA WENYEVITI WA HALMASHAURI YA KINONDONI

 



Na Andrew Chale,

Dar es Salaam.


Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDS) imetoa mafunzo ya uelewa kwa Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Mitaa ya Halmashauri ya Kinondoni tayari kwa zoezi litakaloanza Novemba 21-25 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.



Ambapo Watendaji na Wenyeviti hao, wamepewa mafunzo ya uelewa katika kuelekea kampeni ya ugawaji wa Kingatiba kuthibiti Ugonjwa wa matende na mabusha (Ngirimaji).


Kampeni ya ugawaji wa Kingatiba kuthibiti Ugonjwa wa matende na mabusha (Ngirimaji) inarajiwa kuzinduliwa tarehe 21- 25, Novemba mwaka huu ambapo itafanyika nyumba kwa nyumba katika halmashauri za Temeke, Kinondoni na Ilala Jiji mkoani Dar es Salaam.



MH MARY MASANJA KUONGOZA MBIO ZA 'PANDE TRAIL RUNNING & CYCLING' NOVEMBA 19





NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Mary Masanja anatarajiwa kushiriki tamasha la mbio za hisani za 'Pande Trail Running & Cycling'

Novemba 19 mwaka huu zenye lengo la kuwasaidia watoto wenye ulemavu wanaoishi mitaa inayozunguka Pori la akiba la Pande lililochini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wananyapori nchini (TAWA).


Mh. Mary Masanja atashiriki mbio hizo pamoja na wadau mbali mbali ambapo pia atakabidhi badhi ya vifaa kwa watoto hao.


Kwa mujibu wa Afisa Mahusiano Mkuu wa TAWA, Vicky Kamata, amesema kuwa shughuli hiyo ya kipekee katika Pori la Pande

zimeandaliwa kwa pamoja na TAWA kwa kushirikiana wadau ambao ni Dar Running Club na Taasisi ya Africa Foundation for inclusive Communities (AFIC) ikiwa na lengo kusaidia watoto hao hususani walemavu.


Ambapo kutakuwa na Michezo mbalimbali ikiwemo ya kuendesha Baiskeri na kukimbia katika maeneo hayo yenye Utalii wa msitu huo wa Pande.



"Maandalizi yanaendelea vizuri na Naibu Waziri Mhe. Mary Masanja ndiye atakae kabidhi vifaa hivyo katika hilo la tarehe 19.11.2022." Alisema Vicky Kamata 


Na kuongeza kuwa:

"Mbio hizi tumezipa kauli mbiu ya "Kimbia Mlemavu atembee", hivyo tuungane na Naibu waziri Mhe Mary Masanja, tuungane na TAWA,tuungane na Watoto wenye Ulemavu katika kushiriki Mbio hizi." Alisema.


 Aidha, alisema zoezi la usajili lilikuwa likiendelea Mlimani City, ambapo pia unaweza piga simu: 0788466330 na

0713974398 kwa maelezo zaidi.


Ambapo vifaa vya mazeozi vitanunuliwa kwa ajili ya watoto 36 wenye ulemavu wa miguu ambapo Watoto hao wenye ulemavu wanasimamiwa na Taasisi ya Africa Foundation for Inclusive Communities (AFIC).


Pia mbali na mbio hizo, kutakuwa na mambo mengine mengi kwa washiriki ikiwemo michezo na nyama choma za pori 


TPA KUKAMILISHA MIRADI YOTE YA MABORESHO YA BANDARI YA TANGA IFIKAPO APRILI 2023.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameitaka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kuhakikisha miradi yote ya maboresho ya bandari ya Tanga inakamilika ifikapo mwezi Aprili 2023 ili bandari hiyo ianze kufanya kazi kwa ufanisi na kuruhusu meli kubwa zaidi kuanza kutumia bandari hiyo.

 

Makamu wa Rais amesema hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Gati mbili pamoja na uongezaji kina kutoka mita 3 hadi 13 unaondelea katika Bandari ya Tanga. Amesisitiza ni lazima bandari hiyo iweze kufanya kazi kwa viwango na kuvutia zaidi watumiaji wa bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Pia amemuagiza Meneja wa Bandari ya Tanga kushughulikia haraka malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu utendaji wa bandari hiyo ikiwemo kuchukua muda mrefu utokaji wa mizigo inayopita katika bandari hiyo ikilinganishwa na bandari nyingine za jirani. Amesema mapungufu hayo katika bandari ya Tanga yamepelekea wafanyabishara kutumia bandari za nchi Jirani na hivyo kulikosesha taifa mapato ambayo yangetumika kuwahudumia wananchi.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha uchunguzi unaoendelea wa kuungua moto kwa ghala la mali za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) la forodha. Amesema unahitajika uchunguzi wa kina ili kubaini wote waliohusika katika kusababisha hasara iliojitokeza katika ghala hilo. Pia amewataka viongozi wa TRA kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza mapato pasipo kuwanyanyasa wafanyabishara.

 

Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi mbalimbali mkoani Tanga kuwa na ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinapojitokeza na kuhakikisha wanakomesha biashara ya dawa za kulevya, magendo,uvuvi haramu, uhamiaji haramu pamoja na biashara haramu ya binadamu.

 

Aidha amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga kusimamia wale wote wanaopaswa kujibu hoja zilizoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha wanajibu hoja hizo haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na ubadhirifu wa fedha za umma.

 

Miradi ya Maboresho ya Bandari ya Tanga inagharimu shilingi bilioni 429 na inatarajiwa kuongeza ufanisi kufikia kuhudumia  tani milioni 3 kwa mwaka kutoka tani laki saba na hamsini za sasa.

Wednesday, 16 November 2022

TULIA AKSON MGENI RASMI KONGAMANO LA MABINTI

 

Pichani. Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Victory Celebration Centre liliopo Jijini Dodoma Pasta Josephine Kihoza wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ujio wa Kongamano


Na Deborah  Lemmubi - Dodoma.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson  anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la Wanawake na Mabinti linaloitwa MEGA LADIES TALK SHOW lililoandaliwa na umoja wa VCC Super Ladies kutoka Kanisa la VCC lililopo Jijini Dodoma,  litakalo jumamosi 19/11/2022 lenye kubeba kauli mbiu isemayo: BORN TO WIN AND SHINE.


Hayo yamesemwa na Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Victory  Celebration Centre liliopo Jijini Dodoma Pasta Josephine Kihoza wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ujio wa Kongamano hilo lililolenga kuwa na mkusanyiko mkubwa wa mazungumzo ya Wanawake.


"Ndugu wana habari,Kanisa la VCC kupitia kikundi maalum kinachoundwa na wanawake na mabinti wajulikanao kama VCC Super Ladies tumeandaa kongamano kubwa sana la kihistoria hapa Dodoma litakalofanyika siku jumamosi tarehe 19/11/2022 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni Mabeyo Complex, Kongamano hili linaitwa MEGA LADIES TALK SHOW ikimaanisha Mkusanyiko mkubwa wa mazungumzo ya wanawake. Kwa kifupi Kongamano hili linaitwa MELA TALK au MELA - TALK SHOW"


Aidha Pasta Josephine amesema kuwa licha kongamano hili kuwalenga wanawake na mabinti lakini pia linawahusu wanawake wa dini na kabila zote wa umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kutoka ndani na nje ya Dodoma.


"Talk Show hii inawalenga mabinti na wanawake wa dini zote na umri wowote kuanzia miaka 18 na kuendelea ndani na nje ya Dodoma na Mgeni rasmi ambaye tayari amethibitisha ushiriki atakuwa Mhe Dkt Tulia Ackson Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wanenaji atakuwa Mchungaji Tony Kapola na Mtumishi wa Mungu Lilian Mwasha na mbeba maono Mchungaji Josephine atakayesimamia shughuli nzima"


"Na kuongeza kuwa kauli mbiu ya mazungumzo hayo ni: BORN TO WIN AND SHINE" kwa kiswahili tunasema "NITASHINDA NA KUNG'ARA"


Pia Pasta amesema Kongamano litakuwa ni endelevu na uhitaji ukiwa mwingi watafanya kwa mwaka mara mbili.


"Tunaamini baada ya jumamosi watu watasimulia kwa yote yatakayofanyika katika kongamano hili. Hivyo kongamano hili litakuwa ni endelevu na uhitaji ukiwa mwingi tunaweza kufanya kwa mwaka mara mbili kwani hii ni semina ya mabadiliko"


Nakuahidi kuwa watalifanyia kazi suala kwenda vijijini kufanya makongamano mana huko ndiko tunakotoka wote.


Mela Talk ni matokeo ya maono ambayo Mungu aliweka ndani ya moyo wa Josephine Kihoza, Mama Mchungaji na Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la CAG - VCC Dodoma ya kuendesha semina,makongamano na mijadala mbalimbali ya kuwasaidia na kuwaweka watu huru ili wawe na maisha mema na yenye furaha kama alivyokusudia Mungu.

Tuesday, 15 November 2022

WALIMU 17,000 KUPEWA MAFUNZO YA UONGOZI NA ADEM

 

Pichani: Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dkt.Siston Mgullah, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Na Deborah  Lemmubi - Dodoma.

 ADEM yajipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao 17,000, na kutoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.


Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM)  Dkt.Siston Mgullah, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 ,mbele ya waandishi wa habari leo Novemba 15,2022 Jijini Dodoma.


Dkt.Mgullah amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha wa 2022-2023 wakala hiyo imejipanga kudahili Walimu 2343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.


"Wakala umedahili Walimu 1,839 katika mafunzo ya Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ili kuwapa ujuzi na maarifa walimu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathimini katika elimu"


Na kuongeza kuwa "Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani, kwa Maafisa 3,860 (REOs, RAOs, DEOs, WEOs) ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wenye kuleta tija katika elimu"


Aidha Mtendaji huyo amesema kuwa Wakala hiyo imetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia.


Dkt.Mgullah ameongeza kuwa Wakala pia umeendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Walimu Wakuu na Waratibu wa Taaluma 147 kutoka katika Shule za Msingi na Sekondari Zanzibar, chini ya mradi wa Mwanamke Initiative Foundation (MIF).


Pia ,Wakala umeendesha mafunzo ya Kamati za Shule kwa Washiriki 126 katika Mkoa wa Songwe ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika Shule na umeandaa mtaala wa shahada ya menejimenti ya uthibiti ubora wa elimu ili kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu bora katika ngazi zote za elimu.


"Tumefanya Tafiti sita na tumuwasilisha kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mapungufu na kuandaa mafunzo wezeshi kwa wahusika.Tumeandaa Moduli 3 katika eneo la Uongozi na Usimamizi wa Shule ili kuendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa ujenzi wa umahiri kwa walimu wa Shule za Sekondari Zanzibar na umeandika vitabu vya kujenga umahiri katika utekelezaji wa Mtaala wa Sekondari ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kwa ajili ya Shule za Zanzibar"


Dkt.Mgullah amesema kuwa moja kati ya malengo ya Wakala hiyo ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa elimu bora shuleni kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya elimu, kuziba ombwe la maarifa na ujuzi ambalo kiongozi au mtendaji hakupata katika mafunzo ya awali ya Ualimu na kuongeza idadi ya viongozi wenye maarifa ya uongozi na usimamizi wa elimu.


"Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Wakala umefanya tafiti mbalimbali zikiwemo za tathimini ya matokeo ya Mafunzo ya KKK kwa Walimu wa Darasa la III na IV yaliyofanyika Tanzania Bara, utekelezaji wa uthibiti ubora wa shule na utoaji wa mrejesho kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Msingi"


Pia amesema kuwa wanafuatilia utendaji kazi wa Wakuu wa Shule waliopata mafunzo ya Uongozi na Utawala katika Elimu, wanafuatilia matokeo ya mafunzo ya Stashahada ya uongozi na usimamizi wa Elimu na tathmini ya athari za kozi ya Astashahda ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa elimu iliyofanyika katika mikoa minne.


Kwa Upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali imeweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.


"Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali"


Aidha Msigwa amesema Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hiki ili wakapate ujuzi wa kusimamia vizuri taasisi hizo.


Pia Msigwa ametoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM.


Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM ulianzishwa Agosti 31, 2001 ukiwa na majukumu ya kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa elimu katika ngazi zote na kutoa ushauri wa kitaalamu katika mambo yanayohusu uongozi na usimamizi wa elimu.

SIMBA WAMKANA KOCHA WA MAKIPA MWAHARAMI MOHAMED

 

Pichani: kushoto ni Mwaharami Said Mohamed,katikati Juma Mgunda Kocha wa Muda wa Simba na Kulia Seleman Matola aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba.

Na Mwandishi Wetu.

Uongozi wa Simba kupitia #SimbaApp umeujulisha umma kuwa Kocha wa makipa Muharami Saidi Mohamed “Shilton” (Wa kwanza kushoto) hakuwa mwaajiriwa wa klabu hiyo na hakuwa na mkataba na Simba.


Simba ilimuomba Muharami kuwanoa makipa wake kwa muda wa mwezi mmoja,Wakati klabu ikiendelea kutafuta kocha wa kudumu.


Hivyo klabu haiusiki na tuhuma zinazomkabili Muharami na ipo tayari kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika pindi itakapohitajika kwa maslahi ya taifa.


Aidha Uongozi wa Simba umesema unawaomba mashabiki kuwa watulivu kwani hakuna athari yoyote kwa klabu kufuatia kadhia iliyomkumba Kocha huyo.


Mapema leo ilikuja taarifa kutoka kwa Kamishina Jenerali Bw.Gerald Kusaya kuwa wanawashikilia watu 9 akiwemo Muharami na Alhaji kambi Zubery Seif wa Cambiasso Academy kufuatia kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya Heroin yenye kilo 34.9.

Monday, 14 November 2022

EWURA YAZITAKA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI KUTOA TAARIFA SAHIHI

 

Pichani: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) Mhandisi Modestus Lumato,akizungumza wakati wa kikao kazi cha Watendaji wa Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya Kitaifa kilicholenga kuhakiki taarifa za utendaji wa Mamlaka hizo kwa mwaka 2021/22 kilichofanyika leo Novemba 14,2022 jijini Dodoma.

Pichani: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) Mhandisi Modestus Lumato (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mamlaka za maji na Miradi ya kitaifa mara baada ya kufungua kikao kazi cha Watendaji wa Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya Kitaifa kilicholenga kuhakiki taarifa za utendaji wa Mamlaka hizo kwa mwaka 2021/22 kilichofanyika leo Novemba 14,2022 jijini Dodoma.

Kutoka DODOMA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) Mhandisi  Modestus Lumato, amezitaka Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini kuhakikisha zinatoa taarifa sahihi za huduma ya maji na usafi wa mazingira kwa wananchi ili kushamirisha upatikanaji wa huduma endelevu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.


Mhandisi Lumato ametoa maelekezo hayo leo Novemba 14,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha Watendaji wa Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya Kitaifa kilicholenga kuhakiki taarifa za utendaji wa mamlaka hizo kwa mwaka 2021/22.


Mhandisi Lumato ameeleza kuwa tathmini iliyofanywa na EWURA imebaini kuwapo mamlaka za maji ambazo zimeendelea kuwasilisha taarifa zenye mapungufu kwenye kukidhi viwango vya huduma, uchakavu, ufanisi wa makusanyo wa maduhuli, muda wa upatikanaji wa huduma, ubora wa maji pamoja na idadi ya wananchi wanaopata huduma, hali hii inakwamisha kufanya tathmini ya hali halisi ya utendaji na upatikanaji huduma.


“Nitoe wito kwa mamlaka zote za maji kuhakikisha zinafanya masahihisho kwenye taarifa zenye mapungufu ili ziweze kutoa hali halisi ambayo mwisho wa siku itasaidia katika kupima utendaji na ufanisi wa huduma wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira” amefafanua  Mhandisi Lumato


Kwa upande wake Mwakilishi wa katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Adam Ishara,amezitaka Mamlaka hizo kujitahidi kutekeleza wajibu wake kwa kutoa takwimu sahihi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza kuwa, Wizara ipo tayari kutoa miongozo na ushirikiano unaohitajika muda wowote.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira,ambaye ni Meneja Ufundi wa Maji na Usafi wa Mazingaira EWURA, Mhandisi Titus Safari,amesema kuwa mchakato wa maandalizi ya ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji ni shirikishi hivyo kila mamlaka itumie kikao hicho kuthibitisha usahihi wa taarifa zake.


WATENDAJI  kutoka Mamlaka 25 za Majisafi na Usafi wa Mazingira za miji mikuu ya mikoa na mamlaka 7 za miradi ya kitaifa wamehudhuria kikao kazi hicho kinachofanyika makao makuu ya EWURA jijini Dodoma.

KITENGO KIPYA CHA MAJANGA AJALI KUSHUGHULIKA KATIKA KUOKOA MAISHA YA WATU

 



Na Englibert Kayombo  Dodoma.


Wizara ya Afya imeendelea kuboresha mikakati ya kuokoa maisha ya watu kutokana na majanga na ajali kwa kuanzisha Kitengo mahsusi kitakachoshughulika na kuokoa maisha ya watu kutokana na ajali.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipowatembelea majeruhi wa ajali iliyohusisha Basi la Arusha Express kugongana na Lori eneo la Mzakwe, Dodoma.


“Katika Mipango yetu pale Wizarani, Kitengo cha Magonjwa yasiyoambukiza sasa hivi tutakiita Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza, Ajali na Afya ya Akili”. Amesema Waziri Ummy Mwalimu.


“Ajali zinatokea, lakini ni wajibu wetu ajali zinapotokea kuhakikisha tunatoa msaada wa haraka kwa majeruhi wa ajali, kwa hiyo hili ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele”. Amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu.


Waziri Ummy amesema pia katika Wizara ya Afya ipo Idara ya Utayari na Udhibiti wa Majanga na Magonjwa ya Mlipuko na kuwataka pia kutojikita kwenye kushughulikia magonjwa ya mlipuko pekee bali pia na kuwa na mwitikio wa haraka kushughulikia majeruhi wa ajali.


Waziri Ummy amesema kupitia Idara hiyo, vilianzishwa vituo vya utayari na dharura kushughulikia majanga na ajali pembezoni na barabara kuu kutoka Dar Es Salaam hadi Mbeya hivyo kuwataka watalaam kuwa na mpango huo kwa barabara ya kuelekea Mkoa wa Dodoma.


Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwapa pole majeruhi wote wa ajali hiyo na kuwatakia afya njema na kupona haraka pamoja na kuwapongeza watoa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kuwahuduma vyema wagonjwa na majeruhi wa ajali hiyo.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest amesema Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 22 pamoja na watu 6 waliofariki ambapo kati ya majeruhi hao 1 alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa.


Dkt. Ibenzi amesema katika majeruhi 21 waliokuwa katika Hospitali hiyo, 1 alifariki, watu 9 walipewa ruhusa na 11 wamesalia wakiendelea kupatiwa huduma za matibabu.


ALA ZA MUZIKI ZA MIKOA YOTE ZIKUSANYWE ZIHIFADHIWE MAKUMBUSHO YA TAIFA: DKT.MPANGO


Pichani: Makamu wa Rais Mhe Dkt. Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Elimu wa Makumbusho ya Taifa Bi. Anna Sonelo alipotembelea banda hilo la maonesho TASUBa.
               (Picha na Andrew Chale).


Na. Andrew Chale

Bagamoyo.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Mpango ameagiza Makumbusho ya Taifa kukusanya Ala za Muziki za mikoa yote hapa Nchini ili ziweze kuhifadhiwa kulinda tamaduni za Mtanzania.


Makamu wa Rais Mhe. Dkt.Mpango ametoa kauli hiyo Novemba 11, 2022 wakati akizindua  Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Mkoani Pwani.


Ambapo ametembelea Banda la Makumbusho ya Taifa ambao  wanashiriki tamasha hilo kwa kuonesha Ala mbali mbali za muziki za baadhi ya makabila ya hapa Nchini,

Pia maonesho ya picha jongefu za kale katika masuala ya Sanaa na Utamaduni,


Makamu wa Rais Mhe. Dkt.Mpango pia amepatiwa maelezo namna Makumbusho hiyo inavyofanya kazi zake kwa ukaribu na Wasanii.


Hata hivyo, akatoa agizo hilo, la kukusanya Ala za muziki kwa kila mkoa na hata kuvihifadhi kwani baadhi upotea kutokana na ukuaji wa teknolojia,


Makamu wa Rais Mhe Dkt.Philip ametaka Ala hizo zikipatikana zihifadhiwe angalau ziweze kukaa miaka 200, ili vizazi vijavyo wavijue na kuona umuhimu wa Ala hizo za Muziki wa Tanzania.


Baadhi ya Ala hizo za muziki ambazo zipo hapo ni Zeze, Ngoma, Marimba, manyanga na  zingine nyingi.


UZALISHAJI WA SUKARI KUONGEZEKA TANI 756,000 MWAKA 2025/2026.

 

Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Sukari Tanzania,Prof.Kenneth Bengesi akizungumza Leo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo Pichani) Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023


Kutoka Dodoma

SERIKALI kupitia Bodi ya Sukari Tanzania imesema kuwa Nchi haitakuwa na uhaba wa sukari katika kipindi Cha Miaka miwili ijayo ambapo uzalishaji utaongezeka kutoka Tani 380,000 za Sasa hadi kufikia Tani 756,000 ifikipo Mwaka 2025/2026.


Uhaba huo wa Sukari utaisha katika kipindi hicho kutokana na Mikakati mbalimbali iliyowekwa na bodi hiyo ya kuongeza viwanda vya ndani.

Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Sukari Tanzania,Prof.Kenneth Bengesi ameyaeleza hayo Leo mbele ya Waandishi wa Habari Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Prof.Bengesi amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia suluhu hassan imedhamiria kuongeza uzalishaji wa sukari nchini kwa kujenga viwanda vingi ili kuongeza ajira kwa Watanzania.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kwa sasa Serikali inatumia fedha nyingi kuagiza sukari kutoka nje ya nchi ambapo serikali inatumia zaidi ya dolla million 150 ambazo ni zaidi ya billion 300.

"Serikali inatumia zaidi ya dolla million 150 ambazo ni zaidi ya billion 300 kuagiza sukari nje ya nchi jambo ambalo linawezekana kuzuilika endapo tutadhamiria kwa pamoja kuongeza uzalishaji wa sukari nchini kwa kujenga viwanda vingi jambo ambalo pia litaongeza ajira kwa Watanzania,"Amesema Prof.Bengesi

Na kuongeza kuwa "sisi kama chombo cha udhibiti chenye ufanisi na kinachoweza kuhudumia na kusaidia tasnia ya sukari kufikia ushindani na uendelevu unaotakiwa tuna jukumu la kuisaidia serikali kupunguza gharama za uagizaji wa Sukari kutoka nje na ili tufanikiwe ni lazima tuwekeze kwenye ujenzi wa viwanda,"Prof.Bengesi


Bodi ya Sukari Tanzania kwa kuongozwa na kanuni za kutoa huduma kwa usawa, huduma bora na uadilifu, inalenga kuunda, kudumisha na kudhibiti mazingira ambayo yanawafaa wawekezaji wa sukari kuzalisha miwa, sukari na bidhaa zinazohusiana kwa ufanisi na kwa faida.

RESHAPING INDUSTRIES WITH AI:HUAWEI CLOUD LAUNCHES PANGU MODELS 3.0 AND ASCEND AI CLOUD SERVICES

Zhang Ping'an, Executive Director of Huawei and CEO of Huawei Cloud, announcing Pangu Models 3.0. [Dongguan, China, July 7, 2023] The...