mwambelablog

Friday, 25 November 2022

WILAYA YA KYERWA YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO

 


Na Lydia Lugakila

Kutoka Kyerwa.


Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imempongeza Rais Samia kwa kuwaletea miradi mbali mbali ya maendeleo ambapo wanatarajia ifikapo Novemba 25 ya mwaka mahakama mpya wilaya itaanza kufanya kazi baada ya kukamilika jambo litakalowaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika wilaya jirani ya Karagwe.


Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili taarifa mbali mbali za robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023 kilichofanyika ukumbi wa Rweru mkuu wa wilaya ya Kyerwa Rashid Mohamed Mwaimu amesema kuwa juhudi za Rais Samia zimeifanya wilaya hiyo kuendelea kung'ara kwani kwa kipindi cha muda mrefu wananchi wake wamekuwa wakifuata huduma ya mahakama katika wilaya jirani ya Karagwe ambapo walilazimika kutumia mwendo wa kilometa 80.


"Novemba 25 mwaka huu mahakama yetu inaanza kufanya kazi namshukuru Rais Samia kwa kutusogezea huduma hii, nawashukuru wanakaragwe kwa kutufadhili kwa kipindi chote hicho sasa wilaya yangu inajitegemea inasimama kwa miguu yote" alisema Mwaimu.


Aidha Mwaimu ameongeza kuwa ifikapo Desemba mosi mwaka huu wanatarajia kuanza baraza la nyumba la wilaya baada ya kukamilika kwa ujenzi itasaidia  wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda wilayani Karagwe kufuata huduma hiyo.


Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya amewaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwani hadi sasa wilaya ya Kyerwa imeongezewa nguvu kazi katika sekta mbali mbali ikiwemo afya, Elimu huku akimuomba Rais Samia kuiangalia wilaya hiyo kwa macho mawili kutokana na kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa watumishi.

No comments:

Post a Comment

RESHAPING INDUSTRIES WITH AI:HUAWEI CLOUD LAUNCHES PANGU MODELS 3.0 AND ASCEND AI CLOUD SERVICES

Zhang Ping'an, Executive Director of Huawei and CEO of Huawei Cloud, announcing Pangu Models 3.0. [Dongguan, China, July 7, 2023] The...