Pichani:Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Dkt Daniel Chongolo akizungumza na wanahabari pichani hawapo.
Na Deborah Lemmubi - Dodoma.
Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu wafutiwa Uchaguzi kwasababu ya uwepo wa tuhuma za Rushwa.
Hayo yamesemwa mapema leo hii Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Dkt Daniel Chongolo alipokuwa akizungumza na wanahabari kutoa Taarifa juu ya chaguzi zinazoendelea ndani ya chama cha CCM kwa ngazi ya Mikoa.
"Tumefuta uchaguzi wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu kwa sababu ya kuwepo kwa tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wagombea,nimeshatuma timu huko leo siku ya tatu kufanya uchunguzi wa kina wakimaliza wakatuletea ripoti tutafanya uamuzi"
Aidha Dkt Chongolo amesema kuwa wamesimamisha Uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa kwa Mkoa wa Mbeya na Arusha nayo changamoto ikiwa ni tuhuma za Rushwa.
"Pili tumesimamisha Uchaguzi nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mkoa wa Mbeya kwa sababu ya tuhuma mbalimbali ikiwemo za rushwa na lenyewe tunalifanyia uchunguzi wa kina na tukilikamilisha tutatoa taarifa ya uamuzi wa Chama"
"Tatu tumesimamisha uchaguzi kwa nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mkoa wa Arusha naye tatizo ni hilo hilo changamoto zikiwemo za rushwa,tukikamilisha uchunguzi tutatoa taarifa ya uamuzi wa Chama na kuendelea au kuruhusu Uchaguzi uendelee"
Pia Chongolo amezungumzia malalamiko yaliyojitokeza kwa wagombea kwenye uchaguzi uliofanyika jana Mkoa wa Magharibi kisiwani Zanzibar ambapo amesema.
"Lakini pia kuna uchaguzi uliofanyika jana Mkoa wa kichama Magharibi Zanzibar ambapo kulikuwa na malalamiko ya baadhi ya wagombea na wajumbe wakieleza kuhusiana na tukio la moja ya wanachama kuchukua boksi la kura na kwenda nalo kwenye chumba kilichoandaliwa kwaajili ya kuhesabia kura, sasa kwa sababu tuna haya malalamiko tunataka kujua walilenga kuhesabu kura au walikuwa na lengo lingine na tutafuatilia tukithibitisha tutachukua uamuzi"
Mwisho amewaasa wagombea wanaotumia hila katika Chaguzi zinazoendelea wakionesha kuwa wao ni wagombea maalum na wanaojulikana na viongozi wa ngazi za juu.
"Changamoto tunayopitia hivi sasa ni baadhi ya wagombea au wapambe wao kujionesha kuwa wao ni maalum kuliko wengine na wao ndio wanaojulikana na viongozi wa juu kuliko kuliko wengine wapo wanaojiita wagombea wa Katibu mkuu,wapo wanaojiita wagombea wa Makamu Mwenyekiti, wapo wanaojiita wagombea wa Mwenyekiti na wapo wanaojiita wagombea wa Wajumbe wa Kamati Kuu,waache kutumia hila hiyo katika Uchaguzi"
Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha unaendelea kama kawaida pamoja na nafasi zingine za wajumbe,wawakilishi wa Chama kwenda kwenye jumuiya nyinginezo bado unaendelea kama kawaida.
No comments:
Post a Comment