Imesemwa kuwa sekta ya usafiri wa anga inaendelea kukua kutokana na kuzingatiwa kwa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (ISO 9000:2015) ambapo jumla ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika mwaka 2021/22 ukilinganisha na ndege 35,111 zilizohudumiwa katika mwaka 2020/21 ambalo ni ongezeko la asilimia 13.
Ongezeko hilo linatokana na jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali, pamoja na kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuhakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA, Dkt Hamza Kabelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Novemba 2, 2022 jijini Dodoma .
Aidha Dkt Hamza amesema Mamlaka hiyo imekamilisha kwa asilimia 90 utengenezaji wa mitambo ya rada mbili mkoani Mbeya na Kigoma.
"Kwa sasa TMA tuna rada tatu zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara ambazo zinafanya kazi ya kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga la Tanzania, na kwa sasa tumefikia asilimia 90 za ujenzi wa rada zingine mbili Mkoani Mbeya na Kigoma"
Pia mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia rada hizo yalifanyika kiwandani nchini Marekani.
Dkt Kabelwa amesema, mamlaka hiyo katika mwaka huo 2021/22 iliendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na Jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 45. Pia mamlaka hiyo ilifungua barua za dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya kutengeneza rada hizo. Kukamilika kwa rada hizi kutakamilisha mtandao wa rada Nchini wa kuwa na idadi ya rada sita.
Dkt Hamza ameongeza kuwa kwa upande wa utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu Mamlaka kupitia ofisi zake zilizopo kwenye Bandari za Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika inaendelea kutoa huduma kwa ufanisi.
"Huduma hizi zimechangia kuongezeka kwa usalama na ufanisi wa shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maji ikiwemo usafiri, shughuli za bandari, uvunaji wa gesi asilia,
Na kuongeza kuwa "Katika mwaka 2021/22, idadi ya watumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya maji iliongezeka na kufikia 36,774 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na watumiaji 32,736 waliohudumiwa katika mwaka 2020/21"
Mkrugenzi huyo amesema kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.
"Jukumu lingine la kimataifa ni kusaidia ufuatiliaji wa ubora na upatikanaji wa data za hali ya hewa kwa vituo vya hali ya hewa vilivyo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan ya Kusini kupitia kituo cha Kanda kilichopo Tanzania"
"Matukio mbalimbali ya kutopatikana kwa data yaliripotiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa ajili ya kupata msaada zaidi na pia kiliendelea kutoa ripoti za kila mwezi ambazo zilitumwa kwa nchi za Afrika Mashariki," Ameeleza Dkt.Hamza
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa Wananchi kujenga utaratibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
"Ni waambie tu ndugu zangu ni muhimu sana kutumia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwani ndio zitakazokusaidia siku yako iweje unaweza ukatoka na koti wakati utabiri unaonesha kuwa siku hiyo kutakuwa na jua kali au pengine unaweza kutoka hujavaa sweta kumba siku hiyo kutakuwa na baridi hivyo tujenge utamaduni wa kila asubuhi kabla hujatoka angalia kwanza hali ya hewa itajuaje,"Amesema Msigwa
Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha kumi na nne (14) na sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha tano (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019.
No comments:
Post a Comment