Na Deborah Lemmubi-Dodoma.
Imeelezwa kuwa muitikio wa Wanawake katika kozi za Uhandisi na Urubani bado ni mdogo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT Prof Zacharia Mganilwa wakati akizungumza na wana habari kuelezea utekelezaji na shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023 Jijini Dodoma.
Na kuongeza kuwa hii inatokana na mtazamo wa wanawake juu ya aina ya kozi hizi.
"Unajua Mungu alivyoumba Mwanaume na Mwanamke aliwapa sifa tofauti ambazo wakati mwingine zinaweza kuwa changamoto kwa mtu fulani juu ya aina ya kozi,lakini kozi zingine unakuta ni hamsini kwa hamsini,zingine wanaume wanazidi mfano Urubani na Uhandisi wanawake bado sio wengi kutokana na aina ya kozi"
Aidha Prof Zacharia Mganilwa amesema kuwa Serikali imekopa takriban Shilingi bilioni 49 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji ambacho kina majukumu ya kutayarisha Wataalam wa Sekta ya Usafiri wa Anga.
"Fedha hii imegawanywa katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia Wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar es Salaam kwa gharama ya Shilingi bilioni 21 na baadae tutajenga majengo mkoani Kilimanjaro kwa sababu lazima Marubani wafundishiwe ndani ya Viwanja vya Ndege"
Na kuongeza kuwa "Fedha nyingine itatumika kununua vifaa vya mafunzo, kwa kuwa Kituo kitafundisha Marubani, Wahandisi wa Ndege, Wahudumu Ndani ya Ndege na Waajiriwa wa Viwanja vya Ndege, chuo kimenunua ndege mbili zenye injini moja za mafunzo ambazo ziko njiani kuja Tanzania kwa gharama ya Shilingi Dola za Marekani milioni 1.2,"Prof.Mganilwa
Prof.Mganilwa amesema Katika Mwaka wa Fedha, 2022/23, Chuo hicho kimepanga kununua ndege yenye injini mbili kwa ajili ya wanafunzi kukamilisha mafunzo yao kwa sababu mafunzo ya Urubani yanamtaka mwanafunzi ajifunze ndege yenye injini moja na injini mbili.
"Kumfundisha Rubani mmoja nje ya nchi ni Shilingi milioni 200, hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huu inalifanya Shirika la Ndege Nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu Wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini,
Na kuongeza "Tanzania ina zaidi ya ndege 400 zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya Marubani ni wageni, hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea Urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi na Kwa uwekezaji huu unaofanyika, tuna matumaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania litaweza kuwa Shirika bora kwa Afrika"
Mkuu huyo ameongeza kuwa katika kituo hicho cha Umahiri kinafundisha pia Wataalam wa Usafirishaji wa Reli ya Kisasa, hivyonchi itaweza kupata rasilimali watu stahiki kutokana na wataalam wanaoandaliwa na chuo hicho.
Amesema pia Serikali inaendelea kukuza Uchumi wa Buluu, hivyo kupitia uwekezaji wa mradi wa Benki ya Dunia Chuo hicho kimeweza kusomesha Wataalam wa kujenga meli na kusanifu meli kwa mara ya kwanza tangu kupatikana kwa Uhuru ambapo kuanzia mwaka 2023, vijana watakuwa tayari wamemaliza masomo hayo.
"Kwa mara ya kwanza tangu tumepata Uhuru, chuo kinafundisha pia Diploma ya Uchomeleaji na Uungaji wa Bomba la Mafuta, hii itasaidia tusipeleke tu madereva na kina mama lishe bali tupeleke pia Wataalam watakaokuwa wanachoma bomba la mafuta,
Na kuongeza kuwa "Tuna Kituo kingine cha Umahiri cha Kikanda katika usalama Barabarani ambacho kinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Dola za Marekani Milioni 2.1 kwa mradi wote kikiwa na majukumu ya kufanya utafiti wa sababu za ajali na nini kifanyike pamoja na kufundisha Wakufunzi wa Madereva katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki"
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali iliamua kuwepo na Chuo cha Usafirishaji kwa sababu kuendesha vyombo vya moto ni taaluma na ujuzi na kuna miongozo inayotakiwa kuzingatiwa, kinyume cha hapo ni hatari.
"Safari inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwekeza kwenye maeneo muhimu ya uchumi itategemea sana kuwa na wataalam wetu wa ndani kwani hatuwezi kunufaika na thamani ya miradi yetu kama tunategemea wataalam kutoka nje"
Na kuongeza kuwa "NIT watawezesha vijana wetu kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalan ndege tano zinazotarajiwa kuja nchini, ambapo kwa mwaka 2023, ndege nne zitaingia nchini"
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ni chuo cha elimu ya juu kinachotoa mafunzo kwenye njia kuu zote za uchukuzi na usafirishaji ikiwemo usafiri wa barabara, reli, anga, maji na mifumo ya Mabomba.
===========================================.
No comments:
Post a Comment