Pichani:Dkt. James Kengia aKizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI katika kikao kazi cha Tathmini ya Programu ya utoaji wa Elimu ya Afya.
Kutoka Tanga
Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, kutoa elimu kwa jamii na kuweka mikakati thabiti ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko katika jamii.
Hayo yamesemwa leo Disemba 14, 2022 na Dkt. James Kengia alipozungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI katika kikao kazi cha Tathmini ya Programu ya utoaji wa Elimu ya Afya na Ushirikishwaji wa Jamii katika Majanga mbalimbali ya magonjwa ya mlipuko kinachofanyika mkoani Tanga.
Dkt. Kengia amesema lengo la kikao hicho kinachofanyika chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kuwajengea uwezo washiriki, kufanya tathmini, kubaini changamoto pamoja na kuweka mikakati ya namna bora ya kudhibiti majanga yanayosababishwa na magonjwa ya mlipuko.
"Nitoe rai kwa wataalam wa afya kwa ngazi ya jamii, kuendelea kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko kwa wananchi ili mwananchi aweze kujikinga na magonjwa hayo, katika Ugonjwa wa UVIKO-19 tulishirikiana sana na viongozi wa dini katika kutoa elimu ya tahadhari, tuendelee kushirikiana nao ili tuwe na uwelewa wa pamoja" amesema Dkt. Kengia
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuimarisha miundombinu ya kutoa huduma za afya, kununua vifaa tiba pamoja na kuendelea kuajiri wataalam wa afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Afya kutoka Idara ya Kinga Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya Bw. John Yuda amesema, Serikali inao wataalamu ambao wanafanya utafiti katika kutafuta kinga na tiba sahihi ya magonjwa ya mlipuko ili kudhibiti maambukizi katika jamii hivyo amewataka wananchi kuendelea kuwasikiliza wataalamu wa afya kwa kuchukua tahadhari na kujikinga na magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa tishio wa Ebola ambao upo katika nchi jirani.
Naye Mwakilishi kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bi. Chipole Mpelembe amesema mafunzo hayo ya siku tatu yatasaidia kuongeza weledi na mbinu bora za kuongeza uwajibikaji katika kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha, Wizara ya Afya kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Waratibu Afya Jamii kutoka mikoa 13 ya Tanzania Bara iliyopo katika hatari ya kupata ugonjwa wa Ebola, Wadau wa Maendeleo na Watafiti.
No comments:
Post a Comment