Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Arusha inatarajia kuongeza Program 6 katika masuala ya Usimamizi Rasilimali Watu, Ustawi wa Jamii, Uhasibu na Usimamizi wa fedha, Utawala na Usimamizi wa Serikali za mitaa, Utawala na Usimamizi wa Maendeleo na Usimamizi wa Afya Mazingira, pamoja na kufungua tawi Rungemba -Iringa kwa mwaka 2022/2023.
Hayo yamesemwa mapema leo hii Jijini Dodoma na Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt Bakari George wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.
Na kuongeza kuwa Maandalizi ya program hizi yamezingatia mahitaji ya soko la ajira kwa sasa na umuhimu wa kuandaa wahitimu wenye fikra sahihi na uwezo wa kujiajiri.
"Kwa mwaka 2022/2023 Taasisi inatarajia kuongeza program 6 katika masuala ya Usimamizi wa Rasilimali watu(Human Resource Management ),Ustawi wa Jamii (Social Work),Uhasibu na Usimamizi wa Fedha (Accounting and Finance), Utawala na Usimamizi wa Maendeleo( Public Administration and Management), na Usimamizi wa Afya Mazingira ( Environmental Health Management). Maandalizi ya program hizi yamezingatia mahitaji ya soko la ajira kwa sasa na umuhimu wa kuandaa wahitimu wenye fikra sahihi na uwezo wa kujiaji. Pia mwaka huu 2022/2023, Taasisi imepanga kufungua tawi Rungemba Mkoani Iringa"
Aidha Dkt Bakari amesema mwelekeo unaonesha kuwa mwaka 2022/2023 Taasisi itadahili jumla ya wanafunzi wapatao 3948 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 43 ya wanafunzi kwa mwaka 2021/2022 na kutoa sababu za ongezeko hilo.
"Mwelekeo unaonesha kuwa kwa 2022/2023, Taasisi itadahili jumla ya wanafunzi wapatao 3948 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 43 ya wanafunzi kwa mwaka 2021/2022. Na baadhi ya sababu za ongezeko hilo ni pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika uimarishaji wa elimu kwa ngazi ya msingi na sekondari"
"Sababu nyingine ni umuhimu wa fani ya maendeleo ya jamii katika muktadha wa upatikanaji wa ajira na mawanda mapana ya kuwezesha wanafunzi kukabiliana na changamoto za soko la ajira. Aidha sababu nyingine ni jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi ya Maendeleo ya jamii Tengeru. Mathalani kwa mwaka 2020/2021 Mhe Samia Suluhu Hassan aliipatia Taasisi jumla ya Shilingi 2,700,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa kumbi pacha za mihadhara (Twin Lecture Theater) yenye uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1008 kwa mara moja na hostel ya wasichana ya ghorofa nne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike 584"
"Kwa namna ya pekee kukamilika kwa mradi wa hostel ya wasichana licha ya kuwa utapunguza sana changamoto ya malazi iliyokuwa inakabili wasichana na kuimarisha mifumo ya uangalizi na malezi, mradi huu unakwenda kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato kwa Taasisi ambapo kiasi cha Shilingi 187,440,000.00 kinatarajia kukusanya kwa mwaka kutokana na ada ya malipo ya hostel kwa wanafunzi watakaopangiwa hostel. Sababu nyingine ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi ni upatikanaji wa mikopo kutoka Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB). Mathalani kwa Mwaka 2021/2022,wanafunzi 448 walipata jumla ya Shilingi 1,153,376,000.00 na kwa mwaka 2022/2023 idadi ya wanufaika wa mikopo inatarajiwa kuwa 450 watakaopata jumla ya shilingi 1,158,525,000.00"
Pia Dkt Bakati ameelezea kuhusu mafunzo ya Watumishi wa Taasisi ambapo Taasisi imetenga kiasi cha Shilingi 245,133,000.00 kwaajili ya kugharamia watumishi wapatao 31 kwa mwaka 2022/2023.
"Taasisi imeendelea na jitihada za kuwajengea uwezo watumishi wake ambapo katika kipindi cha mwaka 2021/2022 Taasisi ilitumia kiasi cha Shilingi 183,978,000.00 kugharamia mafunzo ya watumishi 27 katika ngazi ya shahada za awali, uzamili na uzamivu na mafunzo mengine ya muda mfupi"
"Kwa mwaka 2022/2023,Taasisi imetenga kiasi cha Shilingi 245,133,000.00 kwaajili ya kugharamia watumishi wapatao 31 ambao watajiunga na Taasisi mbalimbali za elimu hapa Nchini"
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (Tengeru Institute of Community Development - TICD) ni Taasisi ya Serikali ya Elimu ya juu na kati chini ya Wizara ya Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalum.
No comments:
Post a Comment