mwambelablog

Wednesday, 9 November 2022

SERIKALI YALIPA DENI LA SHILINGI BILIONI 500

 


Na Deborah Lemmubi -Dodoma.


Serikali yalipa Shilingi Bilioni 500 kati ya Shilingi Bilioni 731.40 ikiwa ni madeni yaliyorithiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma PSSSF wakati wa kuunganisha Mifuko mwaka 2018.


Hayo yamesemwa mapema leo hii Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma PSSSF, CPA Hosea Kashimba wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.


"Wakati wa kuunganisha mifuko PSSSF ilirithi madeni ya Serikali yaliyohakikiwa yenye thamani ya Shilingi 731.40 bilioni, mpaka sasa kiasi cha shilingi 500 bilioni kimelipwa na Serikali"


"Pia nirudie kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutambua deni la michango kabla ya 1999 maarufu kama (pre 99 liability) ambalo ni Shilingi 4.60 trilioni kwa kutoa hati fungani maalum yenye thamani ya shilingi 2.17 trilioni. Haya yote yanaleta matumaini ya kuwa na mfuko wenye ustahimilivu na endelevu kwa ustawi wa wanachama"


Aidha CPA Kashimba amesema Mfuko  wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF),unatarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 20 kuwalipa watumishi wa Umma waliondolewa kazini kwa kosa la kughushi vyeti. 


Na kuongeza kuwa wanakadilia kulipa watu zaidi ya 9,000 na kiasi cha Sh. bilioni 20 kitatumika kama malipo ya fedha za michango walizozichangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii katika kipindi chao cha utumishi wa umma.


“Rais alielekeza watumishi hawa waliobainika kuwa na vyeti feki waanze kulipwa fedha zao za michango kuanzia Novemba mosi mwaka huu lakini kinachotakiwa hivi sasa kwa watu wote ambao walikutwa na sakata hili ni kwenda kwa waajiri wao wa mwisho ili kujaziwa fomu ambazo zitaletwa kwetu kwa ajili ya malipo hayo.


“Badala ya kuja PSSSF, wanapaswa sasa kwenda kwa waajiri wao wa mwisho ili kujaziwa fomu hizo na kuzilileta kwetu na sisi tutatoa kipaumbele kwao kwa kulipa ndani ya siku 60 tangu kuletwa kwa madai hayo”amesema CPA Kishimba


CPA  Kashimba amesema gharama za uendeshaji wa mfuko huo zimepungua kwa mwaka kutoka Shilingi bilioni 128.93 mwaka 2018 hadi shilingi bilioni 68.83 sawa na kushuka kwa asilimia 46.61 kutokana na uunganishwaji wa mifuko minne.


Amesema uunganishwaji wa mifuko hiyo minne imeleta uendelevu wa mifuko kwani umenusuru udororaji wa mifuko na kuanzishwa kwa mfuko wa PSSSF ambao umeongeza ufanisi wa utoaji huduma.


Amesema kuwa uunganishwaji huo umeondoa ushindani usio na tija kwani kumekuwepo na mifuko ya pensheni miwili yenye majukumu tofauti ya mmoja kuhudumia sekta binafsi na mwingine sekta ya umma.


"Uunganishwaji huu umewezesha kuwianisha mafao yatolewayo na mifuko ya pensheni ambapo kuanzia Julai 1,mwaka huu wanachama wote wa mifuko ya pensheni wanalipwa mafao ya uzee kwa kutumia kanuni zinazofanana ambazo zinalipa mafao  bora na kuwezesha mifuko"


 CPA Kashimba ameeleza kuwa Mfuko huo unatambua Moja ya changamoto kubwa kwenye jamii ni uelewa mdogo kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii hivyo PSSSF imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wanachama wake ili kuhakikisha sekta hiyo inafanikiwa .


Amesema kuwa ili jitihada za kuhakikisha lengo la kutoa huduma bora linatimia,Mfuko unaendelea kutekeleza mambo mbalimbali yanayolenga kurahisisha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na mtandao wa Ofisi za Mfuko ambapo una Ofisi Kila Mkoa na baadhi ya Wilaya Kwa lengo la kuwa karibu na wanachama.


“Mfuko una kituo cha kupiga simu bure kwa ajiri ya wanachama ambapo huduma hutolewa hadi saa mbili usiku ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa masuala ya yanayohusu huduma mbalimbali za uanachama"


Kuhusu matarajio ya baadae,amesema wanatarajia kuongeza vituo vya uhakiki Katika halmashauri mbalimbali na kuanzisha utaratibu wa kujihakiki kupitia simu janja na kusaidia Kila taarifa ya mwanachama iwe kwenye mfumo.


“Matarajio mengine ni kuhakikisha mifumo ya PSSSF inasomana na mifumo mingine kutoka Taasisi za Umma zinazotoa huduma,kurahisisha uandikishaji wanachama na uletaji wa madai kupitia mtandao na kutumia mifumo mipya ya Tehama kulingana na mahitaji ya Mfuko,”amesema


CPA Hosea ametaja matarajio mengine kuwa ni kubuni mifumo mipya na salama ya TEHAMA kulingana na mahitaji ya mfuko pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA kwa asilimia 85 huku lengo likiwa ni kutumia kwa asilimia 100 ifikapo 2023 katika shughuli za Mfuko hivyo kuboresha utoaji huduma.


Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa, amewataka  watumishi wa umma kuhakikisha kuwa wanafuatilia mara kwa mara waajiri wao kama wanawasailisha michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.


“Wafanyakazi ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa mnafuatilia kama waajiri wenu wanapeleka michango yenu katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kusiwe na shida pale ambapo mtumishi akifika wakati wa kustaafu"

No comments:

Post a Comment

RESHAPING INDUSTRIES WITH AI:HUAWEI CLOUD LAUNCHES PANGU MODELS 3.0 AND ASCEND AI CLOUD SERVICES

Zhang Ping'an, Executive Director of Huawei and CEO of Huawei Cloud, announcing Pangu Models 3.0. [Dongguan, China, July 7, 2023] The...