Pichani: Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya awamu ya sita imeanzisha mkakati mahsusi wa kutambua na kuendeleza kazi za uandishi wa vitabu nchini kwa kuanzisha Tuzo maalum ya Uandishi Bunifu ili kuinua ari ya uandishi na usomaji vitabu.
Akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uzinduzi wa kitabu "Continuity with Vision: The roadmap to Success for President Samia Suluhu Hassan" Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema tuzo hizo zijulikanazo kama "Tuzo ya Mwalimu Nyerere" imeanza mwaka huu ambapo kwa kuanzia inahusisha uandishi wa riwaya na mashairi.
Prof. Mkenda amesema katika mashindano hayo mshindi wa tuzo hizo atapata zawadi ya fedha na kitabu atakachoandika kitachapishwa na kusambazwa katika maktaba na maeneo mengine nchini.
Akizungumzia kitabu kilichozinduliwa "Continuity with Vision: The roadmap to Success for President Samia Suluhu Hassan" amepongeza Taasisi ESAURP kwa kuja na wazo la kuandika kitabu hicho na kwa kuhusisha waandishi wanazuoni wengi ambao wameweza kuandika kwa umakini pamoja na mambo mengine maono ya Mhe. Rais juu ya mageuzi ya mfumo wa elimu kwa kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo na mabadiliko ya Mitaala.
"Nimesoma kitabu hiki na
nimefurahi kuona ambavyo waandishi wametambua maono na kasi ya utendaji wa Rais wetu kama title ya kitabu inavyosema, lakini naamini kitakuwa pia chachu ya kuchochea kasi ya kutekeleza maono hayo na kuendelea kuletea taifa letu maendeleo".
Waziri Mkenda amesema kitabu hicho chenye sura zenye maudhui mbalimbali kuhusu maendeleo ya nchi kimeonesha bayana jinsi ambavyo kazi kubwa inafanyika kimkakati katika Awamu ya Sita na kuongeza kuwa kitakuwa chachu ya kuchochea maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rose Sinyamule amesema amefurahi kushuhudia uzinduzi wa kitabu hicho ambacho kimeandikwa na wasomi huku kikijibu maswali mengi yaliyokuwa yakiulizwa na watu wengi.
"Nimejaribu kukisoma kitabu hiki na kufuatilia maelezo kwa ujumla mnachojaribu kuonesha ni kuwa Wasomi wamesema ndio kwa Rais Samia," amesema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rose Sinyamule
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa ESAURP Ruta Mutakyawa amesema kitabu kilichozinduliwa kina jumla ya kurasa 624, Sura 29 na kimeandikwa na waandishi 45 kutoka Vyuo mbalibali hapa nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)
Akielezea kwa ufupi kuhusu kitabu hicho Mhariri Mkuu Profesa Ted Maliyamkono amesema kitabu hicho kimeandikwa ili kuonesha namna Rais anavyotekeleza kwa vitendo maono yake na kuendeleza ya kiongozi aliyemtangulia.
Mwisho
No comments:
Post a Comment