Pichani: Mhandisi Benard Kavishe wakati akitoa taarifa kwa wanahabari juu ya utekelezaji wa shughuli za Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.
Deborah Lemmubi - Dodoma.
Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Bodi ya Usajili ya Wahandisi Nchini yaweka kipaumbele kudhibiti watu wasio na fani ya Uhandisi, maarufu kama Vishoka.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Msajili Mkuu wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Nchini (ERB) Mhandisi Benard Kavishe wakati akitoa taarifa kwa wanahabari juu ya utekelezaji wa shughuli za Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.
"Katika mwaka wa fedha 2022/2023,Bodi inatarajia kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia vipaumbele kama kudhibiti watu wasio na fani ya Uhandisi (Vishoka) wanaoingilia mifumo ya Bodi ya Usajili na udhibiti wa shughuli za kihandisi hapa Nchini ili kazi zote za kihandisi zifanywe na Wataalam waliosajiliwa na kuidhinishwa na Bodi ya usajili wa Wahandisi"
Aidha Mhandisi Kavishe amesema kuwa uwepo wa Miradi mikubwa ya Kimkakati inayotekelezwa hapa nchini imekuwa manufaa kwa Wahandisi wazawa hasa vijana kupata ujuzi kwani miradi hiyo iliyokuja na Teknolojia mpya.
Mifano ya miradi hiyo ya Kimkakati inayoendelea ni pamoja na Ujenzi wa Reli ya kisasa ya Mwendokasi (SGR) na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambapo imekuwa kama darasa kwa vijana wa kitanzania wanoshiriki katika ujenzi wa Miradi hiyo.
Ambapo Mhandisi Kavishe amesema kuwa ,kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya Wahandisi 33,773, kati yao 26,000 wapo katika soko la ajiri huku wenye leseni za Uhandisi wakiwa ni 10,000 na wengi wao wanashiriki kwa namna moja au nyingine katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa inayoendelea.
"Tanzania tunakadiriwa kuwa na jumla ya Wahandisi 33,773 kati yao 26,000 wapo Sokoni na kati ya hao wenye leseni za Uhandisi wakiwa ni 10,0000 tu ,
Na kuongeza kuwa" Tuna Mafundi sanifu 1,979 na maabara za kihandisi 40 si mnajua mnapotaka kujenga ni lazima eneo lipimwa na iangaliwe pia kwa eneo unalotaka kujenga ni aina gani au ni muundo gani inayostahili kutoakana na mazingira kwa ujumla hapo ndio kazi ya maabara zetu zinaanzia"
Pia amesema kuwa Bodi hiyo imeshasajili Makampuni 398 inayojishuhulisha na masuala ya uhandisi huku makapuni 275 kati ya hayo ni ya ndani ya nchi wakati makampuni 123 yakiwa ni kutoka nje ya nchi.
Mhandisi Kavishe ameendelea kusema kuwa malengo ya Bodi hiyo ni kuongeza ushiriki wa bidhaa za ndani (Local content) katika miradi yote inayoendelea hapa nchini.
"Tutaongeza ushiriki wa bidhaa za ndani katika utekelezaji wa miradi inayoendelea kwa mfano kwa sasa Saruji yote inayotumika katika ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere inazalishwa hapa nchini hivyo malengo ya bodi ni kuona vifaa vyote vinatoka hapa nchini hiyo pia itasaidia sana kuongezea nchi mapato maana watu watauza serikali itapata kodi yake"
Mhandisi Kavishe amesema kuwa Matarajio makubwa ya Bodi hiyo ni kujenga kituo Cha Umahiri Jijini Dodoma,kutokana na kuwepo kwa Vijana wengi wenye mawazo ya kibunifu ila wanakosa namna ya kuendeleza mpaka kufika sokoni ,hivyo kituo hicho kitakuwa eneo sahihi la kuendeleza mawazo hayo.
Kuna vijana wengi wenye mawazo mazuri kabisa ila namna ya kuendeleza inawawia vigumu sana ila tumeona sisi kama bodi suluhisho lake ni kujenga kituo cha umahiri ambapo itatumika kuendeleza vijana na Itakuwa na maabara pia"
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa kwa sasa nchi ina miradi mingi hivyo nafasi ya Bodi ya Wahandisi ina nafasi kubwa katika kutoa ushauri namna gani nzuri ya kutekeleza miradi hiyo kwa uhakika.
"Nafasi ya ERB ni kubwa sana katika maendeleo ya Taifa letu kwani kila penye Mradi unaoendelea ERB wapo na wanathibiti ubora wa kazi na wa Mhandisi anayejenga ule mradi hivyo niwaambieni tu hii ni bodi kongwe na haya majengo mnayoyaona yote kuna Mkono wa ERB"
Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Imeanzishwa Mwaka 1968, ikiwa na majukumu ya Kusajili Wahandisi,kuendeleza wahandisi na kutoa hithibati kwa waandisi , hayo majukumu yote ERB inayatekeleza kwa ajili ya usalama wa nchi na kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele.
No comments:
Post a Comment