Na Deborah kutoka Dodoma.
Shilingi Trilioni 3.8 kutumika katika kugharamia jumla ya miradi 44 ya barabara yenye urefu wa Kilometa 1,523, ikihusisha miradi inayogharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani na inayogharamiwa kupitia Washirika mbalimbali wa Maendeleo.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Eng.Rogatus Mativila wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023, mbele ya waandishi wa habari Jijini Dodoma.
Aidha, Eng.Mativila amesema kuwa mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Msalato unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege na majengo ya abiria unaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika AfDB kwa gharama ya Shilingi Bilioni 360.
"Mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Msalato unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege na majengo ya abiria unaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 360,"Amesema Eng.Mativila
Na kuongeza kuwa " Na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba Oktoba 30,2022 Mhe.Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ataweka jiwe la Msingi katika Mradi huu mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Msalato"
Eng.Mativila amesema mbali na miradi hiyo 44 iliyopo katika hatua mbali mbali ya ujenzi kuna miradi mingine 62 ya barabara iliyopo katika hatua mbalimbali za manunuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
"Barabara hizi 62 ambazo zipo katika hatua ya manunuzi zinajumuisha miradi inayogharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani pamoja na fedha kutoka kwa Washirika wa maendeleo"
Katika hatua nyingine Eng.Mativila amesema kuwa Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS imeanza utekelezaji wa Miradi ya EPC + F yenye urefu wa kilometa 2,533km na Makampuni yaliyokuwa shortlisted yamealikwa tarehe 22 Septemba, 2022 kuwasilisha zabuni tarehe 22 Novemba, 2022.
"Miradi hiyo ni kama ifuatavyo: Kibaha - Mlandizi Chalinze Morogoro (km 205) Expressway, Kidatu Ifakara Lupiro Malinyi Kilosa Mpepo Londo Lumecha/Songea (km 512),Arusha Kibaya Kongwa Road (km 493), Handeni Kiberashi Kijingu Njoro Olboroti Mrijo Chini Dalai Bicha Chambolo Chemba Kwa Mtoro Singida (km 460), Igawa Songwe Tunduma (km 218), Masasi Nachingwea Liwale (km 175), Karatu Mbulu Hydom Sibiti River Lalago Maswa (km 389 na Mafinga Mtwango (Km 81)"
Jumla ya miradi 43 ya barabara yenye urefu wa kilometa 2,021.04 na gharama ya Shilingi Bilioni 9.6 ipo katika hatua mbali mbali za upembuzi yakinifu na usanifu.
Katika mwaka wa fedha 2021/22, kati ya Julai 2021 hadi Mei 2022, jumla ya mikataba 20 inayohusisha miradi ya ujenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege inayogharimiwa moja kwa moja na fedha za ndani na mingine kugharimiwa kwa fedha za Washirika wa Maendeleo ilisainiwa.
Mikataba ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya km 582.455 imesainiwa na mikataba ya ujenzi wa Kiwanja cha ndege Msalato na kumalizia jengo la Kiwanja cha ndege Songwe pamoja na mizani ya Rubana ilisainiwa. Gharma ya miradi yote 20 ni Shilingi Bilioni 1,460.84.