mwambelablog

Friday, 12 May 2023

TANZANIA YANG’ARA DUNIANI MATUMIZI YA TEHAMA SERIKALINI.



Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kushika nafasi ya 26 kidunia na ya pili barani Afrika baada ya Mauritius. Hayo yamebainishwa kwenye utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu ukomavu wa matumizi ya Teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index) Ripoti hiyo ambayo inatokana na utafiti uliofanyika mwaka 2022 katika nchi 198 duniani, inabainisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo ilishika nafasi ya 90. Kwa upande wa Afrika, utafiti huo ulihusisha nchi 49 ikiwemo Tanzania na matokeo yamebaini kuwa, matumizi ya TEHAMA nchini yamepanda na kufikia asilimia 0.86 wakati Mauritius ina asilimia 0.864.Tanzania imepanda kutoka nafasi ya tano mwaka 2021 ambapo ilikuwa nyuma ya Afrika Kusini, Ghana, Kenya and Rwanda hadi nafasi ya pili mwaka 2022. Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa kinara kati ya nchi 13 zilizofanyiwa utafiti ambazo ni Burundi, Comoros, Djibouti, Somalia, Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, Kenya, Uganda, Rwanda, Seychelles na Tanzania ambapo matokeo yanaonyesha kuwa Tanzania imepanda kutoka nafasi ya tatu mwaka 2021 hadi nafasi ya kwanza mwaka 2022. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa mwezi Machi mwaka huu, sekta za elimu, afya, fedha na kilimo nchini Tanzania ni sekta zinazoongoza katika utoaji wa huduma za serikali kupitia TEHAMA na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi. Aidha, ripoti hiyo imebainisha kuwa, mafanikio hayo yanatokana na utayari wa serikali wa kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma, uwepo wa dira mahususi kuhusu sera ya TEHAMA, Sheria, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao, mikakati madhubuti na utekelezaji wake unaosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA). Utafiti huo uliangalia maeneo manne ambayo ni mipango na usimamizi wa TEHAMA serikalini ikiwa ni pamoja na uwepo wa Miundombinu ya Kuhitafadhia Mifumo (Data Centers), Miongozo ya kubadilishana taarifa kwa mifumo ya Serikali na uwepo wa mifumo shirikishi, ushirikishwaji wa wananchi kupitia majukwaa ya kidijitali kwa kupima utaratibu unaotumika kwa wananchi kutoa maoni kwa njia ya kidijitali, majukwaa ya kidijitali yanayotumika kushirikisha wananchi, taarifa za wazi pamoja na tovuti za Serikali.

Eneo la mwisho lililoangaliwa ni uwepo wa nyenzo wezeshi za teknolojia serikalini kwa kuangalia Sera ya ubunifu wa teknlojia, sheria na kanuni, ujuzi katika masuala ya dijitali na programu mbalimbali zinazotumika kuimarisha TEHAMA serikalini.

Aidha, utafiti huo umetaja mifumo ambayo imesaidia kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma nchini kuwa ni pamoja na mfumo wa e-Mrejesho ambao unawawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Taasisi za umma kwa njia ya kidijitali, ili kuwasilisha maoni, mapendekezo, maswali, pongezi au malalamiko yao sambamba na kufuatilia utekelezaji wake ndani ya Taasisi husika.

Mifumo shirikishi katika Taasisi za Umma Vituo vya kuhifadhia Mifumo (Government Data Centers) Mifumo hiyo ni pamoja na Mtandao wa Mawasiliano Serikalini ambao umeziunganisha Wizara, Idara na Wakala 72 pamoja na Halmashauri 77, Kituo cha kuhifadhia data cha serikali, Mfumo wa e-Office ambao huwezesha na kurahisisha shughuli za utawala za kila siku ndani ya Taasisi za umma ikiwa ni pamoja na mzunguko wa nyaraka ndani ya Taasisi.

Mifumo mingine ni huduma za mtandao ambazo hurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi kidijitali, huduma hizo ni pamoja na Ajira portal, Mfumo wa Malipo Serikalini (GePG), Maombi na utoaji wa leseni, hati ya kusafiria n.k. Vilevile, Mfumo wa MGOV ambao ni mfumo jumuishi wa utoaji wa huduma kwa njia ya simu za mkononi Serikalini, mfumo huu unarahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma. Mfumo wa mGOV umeunganishwa na watoa huduma wote wa simu za mikononi nchini Tanzania na unatoa huduma za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kupitia namba jumuishi 15200 na 15201 pamoja na huduma za menyu ya USSD kupitia namba jumuishi *152*00#. Aidha, mfumo wa MGOV unaruhusu Taasisi za Umma kutoa huduma kupitia namba binafsi za Taasisi, mfano wa namba binafsi za Taasisi ni 199 ya Wizara ya Afya inayotoa huduma na taarifa za COVID-19, na *113# ya PCCB inayotoa huduma ya kuripoti matukio ya rushwa. Hadi kufikia Julai, 2022 Taasisi zaidi ya 254 zinatumia mfumo wa mGOV kutoa huduma, baadhi ya huduma hizo ni SMS za manunuzi ya umeme (LUKU), SMS za huduma za malipo ya Serikali (GePG), Huduma za kikodi (TRA), Huduma za Ardhi, Huduma za afya (NHIF, CHF) nk. Pia, Mfumo wa GoVESB ambao ni Mfumo shirikishi unaounganisha mifumo ya Taasisi za Umma kuwasiliana na kubadilishana taarifa, Mfumo huu unatumika kupunguza urudufu wa mifumo pamoja na kurahisishsa utendaji kazi wa taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mingine ni Mfumo wa ukusanyaji wa malipo Serikalini (GePG), Mfumo wa ‘Ajira Portal’ ambao hurahisisha utoaji wa matangazo na maombi ya nafasi za kazi kwa njia ya kidijitali. Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE), Mfumo wa taarifa za Usimamizi wa Ushuru na forodha (TANCIS), Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Watumishi Serikalini (HCMIS), Mfumo wa manunuzi mtandaoni (TANePS) na Tovuti Kuu ya Serikali.

Licha ya kuimarika kwa matumizi ya TEHAMA nchini, ripoti hiyo imebainisha kuwa pengo la kidijitali limeongezeka katika nchi masikini zenye uchumi wa chini na wa kati kutokana na uhaba wa fedha pamoja na kutokuwepo kwa sera madhubuti kuhusu TEHAMA. Utafiti huu umekuwa na manufaa kwa mataifa mbalimbali kwakuwa unaangalia zana zinazotumika katika kuimarisha TEHAMA kwenye mataifa mbalimbali pamoja na kuainisha maeneo yanayotakiwa kuboreshwa zaidi.

EWURA YATOA ELIMU KWA MADIWANI WA JIJI LA DODOMA KUHUSU UMUHIMU WA MATUMIZI YA VYANZO MBADALA VYA MAJI.

Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira EWURA, Mhandisi Exaudi Fatael,akizungumza wakati akifungua mkutano wa madiwani wa jiji la Dodoma  kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliofanyika leo Mei 12,2023 jijini Dodoma.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof Davis Mwamfupe,akizungumza wakati wa  mkutano wa madiwani wa jiji la Dodoma  kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliofanyika leo Mei 12,2023 jijini Dodoma.

Meneja wa EWURA Kanda ya Kati Mhandisi Martin Maurus,aakitoa neno la utambulisho wakati wa  mkutano wa madiwani wa jiji la Dodoma  kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliofanyika leo Mei 12,2023 jijini Dodoma.

 

Sehemu ya Madiwani wakifatilia Mkutano wa madiwani wa jiji la Dodoma  kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa kilichoandaliwa na  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kilichofanyika leo Mei 12,2023 jijini Dodoma.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo,akitoa mada kwa Madiwani wa jiji la Dodoma  kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa  kilichofanyika leo Mei 12,2023 jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira EWURA, Mhandisi Exaudi Fatael,akiwa katika picha ya pamoja na madiwani mara baada ya kufungua  mkutano wa madiwani wa jiji la Dodoma  kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliofanyika leo Mei 12,2023 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

MKURUGENZI wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)  Mhandisi Exaudi Fatael,amewataka Madiwani wa Jiji la Dodoma kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa uvunaji wa maji ya mvua kutokana na hali ya upatikanaji wa maji kwenye jiji hilo kutoridhisha.

Mhandisi Fatael ameyasema hayo leo Mei 12,2023 jijini Dodoma ,wakati  akifungua mkutano wa madiwani hao kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyanzo mbadala vya maji jijini hapa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Mhandisi Fatael amesema kuwa  pamoja na hatua ambazo EWURA imeendelea kuchukua, hali ya upatikanaji wa maji jijini Dodoma, imekuwa si ya kuridhisha na kwamba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa sasa ina vyanzo vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita miliomi 67.1 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni 133.844.

“Hii inapelekea upungufu wa lita milioni 66.744 ya mahitaji ya maji kwa siku. Hata hivyo asilimia 28 ya maji yanayozalishwa hupotea. Kutokana na upungufu huo na maji yanayopotea, huduma ya maji inapatikana kwa wastani wa saa 10 tu kwa siku,”amesema Mhandisi Fatael

Aidha amesema kuwa vyanzo vya maji katika Jiji la Dodoma ni visima virefu ambavyo uzalishaji wake hautoshelezi mahitaji hivyo maji hutolewa kwa mgao kwa wastani wa saa 12 kwa siku.

Mhandisi Fatael,amesema kuwa  utekelezaji wa suala hilo unahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali kama Mamlaka za Serikali za Mtaa katika kutafuta suluhu ya kuimarisha hali ya huduma ya maji.

“Madiwani wanayo nafasi ya kutunga sheria ndogo ndogo, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake na kutoa elimu, inatoa rai kwenu, madiwani, kutoa hamasa kwa wananchi mnaowasimamia katika maeneo yenu, kuweka mikakati ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua, wakati hatua mbalimbali za kuimarisha huduma ya maji zikiendelea kuchukuliwa na DUWASA,”amesema 

Awali Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof Davis Mwamfupe,amesema kuwa Jiji litahakikisha linatumia elimu hiyo ya EWURA ili wananchi kuona thamani ya kila tone la maji na kuyavuna.

''Sisi kama Madiwani wa jiji la Dodoma tunawapongeza EWURA kwa kutoa semina hiyo na tunawaahidi kuwa tutaenda kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuona thamani ya kila tone la maji na kuyavuna''amesema Prof.Mwamfupe

Monday, 8 May 2023

WACHUNGUZI WAPIGWA MSASA KATIKA UCHANGUZI MASUALA YA KIFEDHA NA KIDIGITALI


Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akifungua mafunzo kwa wachunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyohusu Uchunguzi wa masuala ya fedha na Uchunguzi wa kidigitali. Mafunzo hayo yalifanyika leo Mei 8,2023  Jijini Arusha.

Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. John Kaole akitoa neno la utangulizi katika mafunzo kwa wachunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyohusu Uchunguzi wa masuala ya fedha na Uchunguzi wa kidigitali. Mafunzo hayo yalifanyika leo Mei 8,2023  Jijini Arusha.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya Pamoja na wakufunzi pamoja na washiriki wa mafunzo  kwa wachunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyohusu Uchunguzi wa masuala ya fedha na Uchunguzi wa kidigitali. Mafunzo hayo yalifanyika leo Mei 8,2023  Jijini Arusha.

Na.Mwandishi Wetu-ARUSHA

Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao ni wachunguzi wamepatiwa mafunzo kuhusu Uchunguzi wa fedha na uchunguzi wa kidigtali. 

Akifungua mafunzo hayo leo Mei 8,2023 jijini Arusha Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeona ipo haja ya kuwapatia watumishi hao mafunzo hayo kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia katika maeneo mbalimbali kama vile biashara, mifumo ya fedha , na maeneo mengine ambayo yameleta mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wa Serikali na sekta nyingine . 

Mhe. Kamishna alieleza kuwa kutokana na changamoto zilizobainika wakati wa utekelezaji wa baadhi ya majukumu ikiwepo suala la kufanya uchunguzi wa masuala ya fedha na uchunguzi wa kidigitali Sekretarieti ya Maadili imeona ipo haja ya kuwapatia watumishi wake mafunzo hayo ili kupata elimu ya uchunguzi wa kiteknolojia.”Tumeona kuwa ni lazima kujifunza na kuelewa namna ya kufanya kazi kulingana na mifumo hii ya kidigitali kadri inavyobadilika ili kupata matokeo mazuri hasa katika nyanja hii ya uchunguzi” alisema.

Aidha Mhe. Kamishna alisema kuwa matarajio ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa umma katika mafunzo hayo ni kuwapata watumishi ambao wataweza kuwa wakufunzi watakaoweza kuwafundisha watumishi wengine namna ya kufanya uchunguzi wa kifedha pamoja na uchunguzi wa kidigitali katika kukusanya taarifa zinazotokana uchunguzi mbalimbali.”Tumewaleteni nyie wachache ili mkawe waalimu kwa watumishi wengine ambao hawapo hapa” alisema .

Awali akielezea majukumu ya Sektetarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Bw, John Kaole alisema kuwa pamoja na majukumu megine Sektetarieti ya Maadili ina jukumu la kupokea fomu za tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni ya viongozi wa umma na kufanya uchunguzi wa awali wa ukiukwaji wa maadili ambao hubainisha kama kuna vihatarishi vyovyote vya ukiukwaji wa Maadili.”Tunafanya uchunguzi wa awali kwa Viongozi wa Umma na endapo tukibaini kuwa kuna ukiukwaji wa maadili tunawapeleka katika Baraza la Maadili kwa ajili ya uchunguzi wa kina,” alisema.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Afisa Uchunguzi Mwandamizi kutoka Makao Makuu Dodoma Bw. Gideon Mafwiri alisema kuwa watumishi hao wamekua na changamoto ya kukosa weledi wa kutosha katika uchunguzi wa masuala ya fedha na uchunguzi wa kidigitali iliyopekelea kushindwa kupata taarifa sahihi katika uchunguzi wa masuala ya fedha na kidigitali” Tumekutana na baadhi ya viongozi wa umma hususan wafanyabiashara kuendesha biashara zao kimtandao na sisi hatukuwa na uweledi wa kutosha katika eneo hili la uchunguzi hivyo baada ya mafunzo haya ni imani yetu kwamba tutakuwa na weledi wa kutosha katika maeneo hayo,”alisema.

Mafunzo hayo ya siku tano kwa watumishi hao yaliongozwa na waratibu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka Makao Makuu Dodoma.

Monday, 1 May 2023

PROF.MWERA:AFUNGUKA UMUHIMU WA MAFUNZO YA VETA KWA VIJANA NCHINI

Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Prof. Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera, akizungumza na wadau wa sekta ya elimu na walimu katika mkutano wa wadau wa elimu 2023 Mkoa wa Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (kushoto) akimkabidhi cheti Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Prof.Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera, baada ya taasisi hiyo kutoa baadhi ya tuzo za heshima kwa washindi.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Prof. Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera (kulia) akiwa meza kuu na viongozi waliohudhuria mkutano huo. Kutoka kushoto ni Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dk.Baganda Elpidius, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, Katibu Tawala Tawala, Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Lucy Boniface na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, Lucia Mwiru.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Prof.Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera, akiwa na Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dk.Baganda Elpidius baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera (kulia) akiwa kwenye mkutano huo.
Wadau wa sekta ya elimu na walimu wakiwa kwenye mkutano huo.
Taswira ya makutano huo.

Na.Alex Sonna-SINGIDA

MKURUGENZI wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Professor Mwera Foundation,Hezbon Mwera ameitaka jamii kuwapeleka katika Vyuo vya Ufundi wanafunzi waliomaliza au wanaosubiria matokeo ya kidato cha nne na darasa la saba ili waweze kusomea kozi za muda mfupi ambazo zitawasaidia kuongeza utaalamu Pia,ameiomba serikali kuanzisha mfuko wa elimu katika kila Halmashauri lengo likiwa ni kusimamia ubora wa elimu.

Prof.Mwera ameyasema wakati akizungumza na walimu hao kwenye mkutano wa wadau wa elimu mkoa wa Singida wa mwaka 2023 ambapo amesema kwa kusoma kozi za muda mfupi zitawaongezea sifa mbalimbali katika utendaji kazi wao katika miaka ya baadae. Pia ameziomba Halmashauri kuanzisha mfuko wa elimu kwani utasaidia kuweka sawa ubora wa elimu pia kusaidia vijana wenye uhitaji ndani ya halmashauri zao. Vilevile, amesema wazazi wana jukumu la kuhakikisha mwanafunzi anapata chakula kipindi anachokuwepo shuleni ili kumfanya azidi kuelewa kwani baadhi hushindwa kufanya vizuri kutokana na njaa. “Utoaji wa chakula sehemu zingine wameanza na uji,hili ni suala muhumu,siku moja muwaite wazazi kwenye kikao muwashindishe na njaa kuanzia asubuhi mpaka jioni ili waone umuhimu wa watoto kupatiwa chakula shuleni. “Mwingine unamwelewesha lakini anaona serikali ina wajibu wa kufanya kila kitu ikiwemo kutoa chakula hapana, Serikali haiwezi kufanya kila kitu,” amesema Mkurugenzi huyo. Mkurugenzi huyo amesema mpaka sasa wamewasaidia vijana zaidi ya 3500 ambao kibajeti ni zaidi ya shilingi bilioni 3 kupata elimu ya ufundi bure bila malipo toka 2019 mpaka sasa kupitia chuo cha Tarime VTC Chenye usajili namba REG/NACTVET/0587 Kinachomilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera Foundation. Amesema pia wanawasaidia watoto yatima ambao wanaishi katika mazingira magumu kuanzia elimu msingi sekondari pamoja na vyuo vya ufundi. “Tunafursa ya kusaidia wale wanaotoka katika mazingira magumu ili waweze kufikia malengo.Maisha haya tunaishi kwa ajili ya binadamu wenzetu.Mipango tunayoweka hatuwezi kufanikiwa pasipo kupitia kwa binadamu wenzetu. Tunapotamani kushikwa mkono nasi pia lazima tushike mkono watu wenye uhitaji.. tutendee watu yale tunayotamani kutendewa pia. “Haya tuliyofanya inawezekana tukashindwa kuona faida yake kwa sasa, lakini kizazi kijacho kitakuja kufurahi kwa haya tunayoyafanya kwa sasa. “Sisi tunasisitiza vijana kujiunga na vyuo vya ufundi na mwaka jana zaidi ya vijana 500,000 waliofanya mitihani waliopata divison one mpaka three ni zaidi ya 150,000, division Four mpaka ziro ni zaidi ya nusu ya waliofanya mtihani,” amesema Prof.Mwera Amesema vijana hao wako wapi wanafanya nini, hivyo ni lazima wahakikishe wanaenda katika vyuo vya ufundi ambayo vitawasaidia kupata ujuzi badala ya kupotelea mitaani na kuingiza Serikali hasara ya kurasimisha mafunzo yaliyopatikana nje ya mfumo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Serikali kupitia Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeipatia kibali Taasisi ya Professor Mwera Foundation kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi Stadi Nchi nzima kazi ambayo tayari inaendelea.

Friday, 28 April 2023

ROYAL TOUR YAONGEZA MAPATO NA KULETA HAMASA KWA WATALII DUNIANI.

 Na Deborah Lemmubi - Dodoma.


Pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na Mwenyekiti Kamati ya Kutangaza Tanzania Royal Tour Dkt.Hassan Abbasi akizungumza na waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Habari Maelezo Jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na Mwenyekiti Kamati ya Kutangaza Tanzania Royal Tour Dkt.Hassan Abbasi amesema mapato ya utalii yameongezeka maradufu kutokana na watalii kuongezeka nchini ikiwa ni matunda ya Royal Tour, ambapo mapato ya jumla ya sekta ya utalii yameongezeka kutoka Trilioni 3.01 mwaka 2021 hadi Trilioni 5.82 na kuifanyaTANAPA na NCAA kuvunja rekodi ya mapato.


Dkt Abbasi ametoa Takwimu hizo Aprili 28,2023 Jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio kumi ya mwaka mmoja tangu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipozindua filamu ya Royal Tour jijini Arusha na hatimaye watanzania wengi kuiona kwa mara ya kwanza filamu ya “TANZANIA; THE ROYAL TOUR"


Aidha ameeleza jinsi ROYAL TOUR ilivyojenga hamasa kwa watalii na wawekezaji, sasa hamasa hiyo pia imekuwa na manufaa kwa sekta ya usafiri wa Anga kama takwimu za Manufaa kwa Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro pekee kama sampuli ya ndege za Kimataifa Zaongeza Ruti Tanzania Miruko ya jumla ya ndege za kimataifa KIA iliongezeka kwa asilimia 28 kutoka miruko 6,115 April 2021 hadi 7,850 April, 2023.


"kutokana na watalii kuongezeka nchini ikiwa ni matunda ya Royal Tour, mapato ya jumla ya sekta hii yameongezeka kutoka Dola za Marekani 1.310.34 (Sawa na TZS Trilioni 3.01) mwaka 2021 hadi Dola za Marekani,527.77 (sawa la TZS Trilioni 5.82) imefanya Tanapa na NCAA wamevunja rekodi ya mapato".


Dkt Abbasi Amesema Royal Tour sio mwisho ni mwanzo wa kuitangaza nchi kimataifa zaidi hivyo Kamati ya mwaka mmoja sasa, imepokea na inaendelea kuchambua “Royal Tours” nyingine zijazo na Maombi Kujitangaza Ligi Kubwa za Ulaya na Marekani Kutokana na hamasa ya Royal Tour klabu mbalimbali za Ligi Kubwa Duniani hasa Uingereza, Hispania na Marekani wapo katika mazungumzo nazo na wameshapokea ofa zao


Ushiriki wa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan  katika filamu ya Royal Tour umeleta mafanikio ambapo Novemba mwaka jana huko Dallas,Texas, USA, Taasisi ya Tuzo za Afrimma ilimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Rais Mwanamke wa kwanza Afrika Kushinda Tuzo ya Mageuzi Katika Uongozi wakitamka bayana kuwa mojawapo ya vigezo na mafanikio ni ushiriki wake katika Royal Tour".


Mpaka kufikia Sasa kuna  wastani wa takribani watu Bilioni 1.2 wamejihusisha na Royal Tour iwe ni kwa kuona,kusikia,kuangalia au kuambiwa na mtu mwingine habari za Makala hii ya Royal Tour.

Wednesday, 26 April 2023

ZAIDI YA WATU MILIONI 2.9 HUPOTEZA MAISHA KUTOKANA NA AJALI NA MAGONJWA YATOKANAYO NA KAZI.

 

Pichani,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira, na Wenye Ulemavu Mhe Prof.Joyce Ndalichako akizungumza na wanahabari jijini Dodoma Leo Apr 26,2023.

Na Deborah Lemmubi - Dodoma.


Takwimu za kidunia  zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani (I.L.O) za mwaka 2022 zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni mbili na laki tisa (2.9) hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yanayotokana na kazi.



Pia zaidi ya wafanyakazi milioni 402 huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona


Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari leo  Aprili 26,2023 Jijini Dodoma kuelekea Maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahala pa kazi,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira, na Wenye Ulemavu Mhe Prof.Joyce Ndalichako amesema Kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217.



"Takwimu hizo ni kubwa sana zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya Wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati wafanyakazi walioumia wakiendelea kupata matibabu. Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo".


Serikali ya JMT inatambua umuhimu wa kulinda Nguvu Kazi ya Taifa. Kupitia Taasisi yake ya OSHA

Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 miongoni mwa wadau na Watanzania wote kwa ujumla. Lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi Nchini yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi".


Ambapo Prof.Ndalichako amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa Mkoani Morogoro katika viwanja vya Tumbaku Aprili 28,2023 na Lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na kuweka mazingira salama katika sehemu za kazi miongoni mwa wadau kupitia kauli mbiu mbali mbali ambazo hutolewa na Shirika la Kazi Duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi” (A Safe and Health Working Environment is a Fundamental Principle and Right at Work).


Kauli mbiu hiyo inatokana na Azimio la Wanachama wa Shirika la kazi Duniani (ILO) katika kikao cha Juni 2022 kilichofanyika huko Geneva Uswisi, na kuamua kuwa suala Usalama na Afya mahali pa kazi liwe mojawapo ya Kanuni na Haki tano za msingi kwa wafanyakazi mahali pa kazi,"



Na kuongeza kuwa "Kanuni na Haki nyingine za msingi

kwa wafanyakazi ni uhuru wa kujumuika na haki ya majadiliano kazini; kukomesha aina zote za kazi ya kulazimishwa; kukomesha ajira za watoto; na kuondolewa kwa ubaguzi katika suala la ajira na kazi".


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa moja kati ya eneo ambalo ajali nyingi zinaripotiwa ni katika sekta ya Uzalishaji ambapo imeajiri vijana wengi huku wengine wakiwa hawana ujuzi wa kutosha katika nafasi wanazofanyia kazi.



"Ukweli ni kwamba eneo la Uzalishaji lina matukio mengi ya ajali na hii ni kutokana na vijana wengi kujikita katika eneo hilo kujiajiri ama kuajiriwa huku wengine wakifanya tu bila kuwa na ujuzi wa kutosha au taaluma kwani eneo hilo mara nyingi wanaangalia nguvu sana kuliko taaluma ndio maana ajali zinakuwa nyingi".


Bi.Mwenda ameongeza kuwa OSHA imejipanga vyema kuelekea maadhimisho hayo ya 19 ambapo washiriki wote watapatiwa Mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.



"Pia OSHA tutajikita katika kutoa mafunzo kwa Sekta binafsi na zile zisizo rasmi kwa sababu wengi hawapo kwenye mfumo jambo ambalo linawafanya kuwa katika mazingira hatarishi na kufanya kazi bila kuzingatia sheria za usalama na afya mahali pa kazi".


Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ilianza mwaka1996 Nchini Marekekani Katika Jiji la New York, ambapo waathirika wa watu walioumia na kupoteza maisha wakiwa kazini hukumbukwa. Maadhimisho hayo yalikuwa yakifanywa na Chama Cha Wafanyakazi Duniani. Ilipofika mwaka 2001,Shirika la Kazi Duniani liliona kuwa ni busara kubadilisha madhumuni ya siku hiyo na kuiita “Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani.


Pia haya ni Maadhimisho ya 19 kwa Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza tulianza kuadhimisha mwaka 2004.

Wednesday, 19 April 2023

SERIKALI INAFANYA MAGEUZI KATIKA SEKTA YA ELIMU

 

Serikali inafanya mageuzi katika sekta ya elimu kwa kuwa na sera na mitaala itakayowezesha wahitimu kuwa na Maarifa, Stadi, ujuzi utakaowawezesha kujiamini, kujiajiri na kuajirika katika mazingira ya utandawazi na kukidhi mahitaji ya soko.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo wakati akimuakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika uzinduzi wa Mkutano wa 31 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara uliofanyika jijini Arusha.

Katibu Mkuu huyo amesema wizara inaendelea kutekeleza vipaumbele vilivyoinishwa katika bajeti ya mwaka 2022/23 ambavyo ni mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Sheria mbalimbali, mabadiliko ya Mitaala pamoja na kuangalia suala zima la idadi na ubora stahiki wa walimu, wakufunzi na wahadhiri pamoja na mahitaji ya miundombinu na vitendea kazi.

“Nitoe rai kwa Menejimenti, Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara na Watumishi wote kwa ujumla kwa pamoja tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha kuwa tunafanya kazi kwa bidii, weledi na nidhamu ya hali ya juu katika kutekeleza majukumu ya wizara yetu kwa ufanisi ili elimu inayotolewa nchini iwe katika kiwango bora na cha ushindani kitaifa na kimataifa” amesema Katibu Mkuu huyo

Prof. Nombo ameongeza kuwa wizara imeshafanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na imekamilisha Rasimu ya Sera toleo la Mwaka 2023, ambapo kwa sasa inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau ili kukamilisha mchakato wa uandishi wa Sera Elimu na Mafunzo itakayozingatia mahitaji ya jamii na soko la ajira la ndani na nje pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Aidha, amewataka watumishi wa wizara hiyo kutumia mafunzo mbalimbali wanayopata kufanya kazi kwa umahiri katika kusimamia na kushiriki ipasavyo katika hatua zote za utekelezaji wa Sera na Mitalaa inayohuishwa ili kuleta tija katika kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia jambo ambalo litawezesha vijana kuwa na uwezo, ujuzi, maarifa, umahiri na ubunifu stahiki na kuweza kuingia katika ushindani wa soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongela ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika katika mabadiliko ya mitaala na mapitio ya Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo yanalenga kuwajengea vijana wa kitanzania umahiri na ujasiri utakao wawezesha kushindana katika soko la Dunia la ajira.

Mhe. Mtahengerwa amewaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa Serikali inatambua uwepo na mchango wa mabaraza ya wafanya kazi nakuwataka kuwa watetezi wa watu na kuacha kutumika kisiasa, huku akisisitiza umuhimu wakutumia lugha za staha wakati wa kuwasilisha hoja na mambo muhimu yanayolenga kuinua hali za wafanya kazi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula amesema baraza la wafanyakazi ni matokeo ya sera ya kuwashirikisha wafanyakazi mambo mbalimbali yanayotokea kwenye maeneo ya kazi, hivyo uwepo wa mkutano huu ni utekelezaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya ushirikishwaji na majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma.

Naye Katibu wa Baraza hilo Huruma Mageni amesema kauli Mbiu ya Mwaka 2023 ya Baraza hilo ni “Sera na Mitaala Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, kauli ambayo inasadifu umuhimu wa kuwa na mitaala pamoja na Sera zinazoendana na mahitaji ya sasa ya sayansi na teknolojia ili kuwafanya vijana wa kitanzania kuajirika na kujiajiri

RESHAPING INDUSTRIES WITH AI:HUAWEI CLOUD LAUNCHES PANGU MODELS 3.0 AND ASCEND AI CLOUD SERVICES

Zhang Ping'an, Executive Director of Huawei and CEO of Huawei Cloud, announcing Pangu Models 3.0. [Dongguan, China, July 7, 2023] The...